![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2020/10/A-14-1024x768.jpg)
Katibu wa CCM Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Ally Kidunda akimnadi Mgombea udiwani wa Kata ya Ngorika Albert Msole.
…………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WAGOMBEA udiwani wa Kata nane kwenye Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, kupitia CCM, wamepita bila kupingwa kati ya Kata 18 za eneo hilo, hivyo kuwa na uhakika wa ushindi kwani ni Kata 10 pekee zilizobakia ambazo zina upinzani kwenye uchaguzi mkuu.
Katibu wa CCM Wilayani Simanjiro, Ally Mohamed Kidunda ameyasema hayo kwa Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Tabia Mwita kwenye mkutano wa kampeni ya kata za Msitu wa Tembo na Ngorika.
Kidunda alizitaja kata hizo nane ambazo madiwani wa CCM wamepitwa bila kupingwa ni Mirerani, Naisinyai, Shambarai na Terrat.
Amezitaja kata nyingine ambazo madiwani wake kupitia chama hicho wanasubiri kuapishwa baada ya kufanyika uchaguzi ni Loiborsiret, Komolo, Oljoro namba tano na Emboreet.
Amesema chama hicho kina uhakika wa kushinda kwani hadi hivi sasa wana mtaji huo wa madiwani nane kibindoni wanatafuta kura za madiwani 10 waliobakia na kupingwa na wapinzani.
“Kwa hapa Ngorika tuna uhakika wa ushindi kwani mgombea wetu Albert Msole ni diwani makini ameweza kuwa Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro kwa miaka minne mfululizo,” amesema Kidunda.
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Tabia Mwita amewaomba wananchi wa eneo hilo kuwapigia kura wagombea was CCM wa udiwani, mgombea ubunge Christopher Ole Sendeka na urais Dk John Magufuli.
“Tunapaswa kutambua kazi kubwa aliyofanya Rais Magufuli kwenye kipindi cha miaka mitano ya kwanza hivyo tumpe nafasi nyingine ya miaka mitano amalizie miradi mingi aliyoianzisha,” amesema Mwita.
Mgombea udiwani kata ya Ngorika Albert Msole amesema kwa kipindi cha miaka mitano ya 2015/2020 amefanikisha miradi mingi ya maendeleo katika sekta mbalimbali hivyo anaomba miaka mitano tena.
Mgombea udiwani kata ya Msitu wa Tembo Kaleiya Mollel amewaomba wananchi wa eneo hilo kutoa kura kwa CCM kwani Tabia ametoka Zanzibar ili aombe kura kwao wasimuangushe.