Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa walikamatwa juzi katika Wilaya za Magu na Ukerewe kwa nyakati tofauti.
Alisema Oktoba 20, mwaka huu, majira ya 12:30 jioni katika kituo cha mabasi, Kata ya Magu Mjini,wilayani Magu, polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya dola walifanikiwa kuwatia mbaroni watu watatu wakiwa na kadi 49 za kupigia kura za wananchi mbalimbali.
Muliro alisema kitendo hicho ni kinyume cha matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2018, kifungu cha 48b kinachoakataza mtu kumiliki na kushikilia kadi ya mpiga kura isiyo yake na kuwanyima watu wengine haki ya kupiga kura .
Kmanda huto wa polisi aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni mgombea udiwani katika Kata ya Kabila (CHADEMA),Peter Malemi maarufu Butage (59),Katibu Kata wa chama hicho, Shija Kimwaga almaarufu kama Mbunda (34) mkazi wa Kijiji cha Igombe na Kulwa Patrice maarufu Sawasawa (34), mkazi wa Magu mjini.
Alisema jeshi l polisi halitasita kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaokiuka na kuvunja sheria za nchi zikiwemo za uchaguzi hivyo watuhumiwa waliokamtwa na kadi hizo za wapiga kura mbalimbali watafikishwa mahakamani ili mfumo wa sheria ufanye kazi yake haraka.
Pia Muliro alisema wanamshikilia Getruda Faustine (43), mkazi wa Kijiji cha Chibasi, Kata ya Nyamagana, Tarafa ya Ukara wilayani Ukerewe, akidaiwa kumkeketa sehemu za siri mtoto mchanga mwenye umri wa siku tisa na kumsababishia maumivu makali.