Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera akiwa ameketi na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Jamillah Yusuf katika hafla ya kukabidhi mikopo kwa wajasiriamali
Baadhi ya wajasiriamali wakifatilia
…………………………………………………………………………………………..
Na Zillipa Joseph, Katavi
Halmashauri ya manispaa ya mpanda mkoa wa Katavi imefanikiwa kukopesha jumla ya shilingi 613,800,000/= kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2019/2020
Akitoa taarifa ya utoaji wa mikopo na mwarejesho hadi mwezi Oktoba 2020 MAfisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Mpanda Bi. Marietha Mlozi amesema vikundi 147 vya wanawake vilikopeshwa 399,300,000/-; vikundi 95 vya vijana vilipata shilingi 198,000,000/- na vikundi sita vya watu wenye ulemavu vilipata mikopo ya shilingi 16,500,000/-
Bi. Mlozi ameongeza kuwa katika msimu huu wa mikopo jumla ya shilingi 155,000,000/- zinatolewa kwa vikundi 37 vya wajasiriamali fedha ambazo zinatokana na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda
Pia ametaja changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na mikopo kutokulipwa kwa wakati ambapo wamelazimika kuwafikisha katika vyombo vya dola baadhi ya wadaiwa sugu
“Tuliwapeleka wadaiwa Polisi huku wadaiwa wengine wakiitwa kuhojiwa na TAKUKURU na kufanikiwa kurejesha sh. 546,282,000/-“ alisema Mlozi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Michael Nzyungu amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kama walivyopanga katika kujiongezea kipato na kuwa waaminifu
Nzyungu ameongeza kuwa halmashauri ina utaratibu wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali kila baada ya miezi mitatu ambapo wastani wa chini wa ukusanyaji mapato kwa mwezi ni shilingi milioni ishirini
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mikopo hiyo mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera amesema mpango huo unaotekelezwa chini ya serikali ya Dokta John Pombe Magufuli unalenga kuwainua wananchi
Sanjari na hilo ameongeza kuwa mkoa una mikakati kadhaa ya kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa, kiwanda cha kutengeneza maji safi ya kunywa na kiwanda cha sukari kupitia wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuwapatia wanachi ajira