Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo, akiwa na viongozi wa Benk ya Biashara ya DCB wakati wa hafla ya utoaji gawio kwa wanahisa wa benki ya biashara ya DCB iliyofanyika kwenye jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………….
Na. Majid Abdulkarim, Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo, ameipongeza benki ya DCB kwa kuingiza faida ya shilingi bilioni 2.1 mwaka wa fedha ulioishia mwaka 2019 na hivyo kuweza kutoa gawio kwa wanahisa wake.
Mhe. Jafo ametoa hizo hivi karibuni kwenye hafla ya utoaji gawio kwa wanahisa wa benki ya biashara ya DCB iliyofanyika kwenye jijini Dar es Salaam.
Aidha Mh. Jafo kwenye hafla hiyo amesema amefurahi kusikia kuwa halmashauri za jiji la Dar es Salaam ambazo ni wanahisa wakubwa wa benki ya DCB zimepata mgao.
Benki ya DCB imetoa gawio la shilingi milioni 500 kwa wanahisa wake wote na wanahisa waliopokea ni Halmashauri za Manispaa na Jiji shilingi milioni 138,603,889 Mfuko wa UTT shilingi 119,074,887 na Shirika la NHIF shilingi milioni 30,780,000.
“Naomba nichukue nafasi hii kuipongeza benki ya DCB kwa mafanikio makubwa iliyoyapata kwa kipindi cha miaka kumi na nane tangu kuanzishwa kwake. Natambua kuwa benki hii imeanzishwa kwa malengo ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wananchi wa kawaida ili wajikwamue kutoka kwenye umasikini”, ameeleza Mh. Jafo.
Vile vile Benki ya DCB imeweza kujiendesha kwa faida kwa miaka takribani 12 kwa ujumla, huku ikitoa gawio kwa wanahisa wake kwa miaka kumi mfululizo, kiasi kinachofikia shilingi bilioni 12 na pia napenda kutambua juhudi za bodi ya wakurugenzi na uongozi wa benki kuhakikisha benki inapata mtaji kupitia zoezi la uuzwaji hisa lililokamilika kwa mafanikio makubwa mwaka jana.
““Napenda kuchukua nafasi hii pia kuwapongeza wanahisa wote wa benki, zikiwemo manispaa za Dar es Salaam, kwa kuiamini benki hii na kuwekeza mtaji tangu benki inaanzishwa, na kuendelea kuwekeza kila mara inapohitajika”, ameongeza Mhe. Jafo.
Pia Mhe. Jafo amesisitiza kuwa serikali inaamini kuwa Sekta ya benki ni kati ya sekta muhimu katika kuendeleza uchumi wa Taifa na wananchi kwa ujumla hivyo mafanikio ya sekta za kifedha nchini ni moja ya nyenzo muhimu katika kufanikisha adhma ya serikali ya kuwa na uchumi imara sambamba na mkakati wa maendeleo wa miaka mitano 2017-2021 ambao unasisitiza juu ya umuhimu na mchango wa sekta ya fedha katika kuchochea shughuli za uwekezaji na uzalishaji mali.
Lakini pia Mhe. Jafo ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na menejimenti ya Benki ya Biashara ya DCB kwa uongozi mahiri na hatua makini katika kuhakikisha benki yenu inaendelea kuwa na kimbilio la wananchi.
Hivyo ni matumaini yetu kama serikali kuwa DCB itazidi kufanya vizuri mwaka hadi mwaka na kuzidi kuboresha huduma zake za kibenki ili ziendane na hali halisi ya watanzania wenye vipato vyote”, ameongeza Mhe. Jafo.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki ya Biashara ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro, amesema kiasi cha shilingi milioni 500 kimetolewa kama gawio kwa wanahisa wa benki hiyo kufuatia idhini ya benki kuu na azimio la wanahisa kupitia ushauri wa bodi ya Wakurugenzi wa benki.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa amesema benki hiyo imeendelea kupata faida kwa mwaka wa tatu na ndio maana imefanikiwa kutoa gawio kwa wanahisa wake.