Meneja miradi Tamwa-Zanzibar Bi Asha Abdi Makame alipokua akifungua mafunzo ya siku moja kwa watototo ambao ni wahanaga wa matukio ya udhalilishaji ambapo mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo katika kutoa ushahidi. Mkufunzi wa maswala ya saikolojia Asya Saleh Abdulatif akifafanua jambo juu ya madhara ya udhalilishaji ambayo wanawaweza kupata watoto wasipowekwa karibu na wazazi wao.
Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) Khamis Juma akieleza ni kwanamna gani kesi za udhalilishaji zinavyohitaji ushahidi kutoka kwa wahusika wenyewe.
************************************
Na Muhammed Khamis,Tamwa-Zanzibar
Wazazi na walezi ambao watoto wao wamewahi kufanyiwa udhalilishaji wa kijisia Zanzibar wametakiwa kutokata tamaa na kuachia matendo hayo yakiendelea badala yake wahakikishe wanafuatilia kwa kina kesi zao ili wahusika waweze kuchuliwa hatua.
Kauli hio imetolewa na Meneja miradi Tamwa-Zanzibar Asha Abdi Makame wakati alipokua akifungua mafunzo ya siku moja kwa baadhi ya watoto waliofanyiwa udhalilishaji kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja.
Alisema kila mzazi ama mlezi anapaswa kufahamu kuwa ni wajibu wake kujitoa na kufuatilia bila ya kuchoka kesi za watoto wao ambao wamefanyiwa udhalilishaji kwani kutotoa ushirikiano katika vyombo hivyo ni kusababisha kutotendeka kwa haki na hatimae watendaji wa matukio hayo kuendelea kufanya kila leo.
Sambamba na hayo aliwataka wazazi hao kufahamu kuwa wanawajibu wa kutoa taarifa sehemu husika na kucha kabisa kuficha taarifa za matukio ya udhalilishaji kwa kuwa kufanya hivyo kutaendelea kusababisha matokea kuendelea.
Katika hatua nyengine akizungumza na watoto ambao wamewahi kufanyiwa udhalilishaji na kesi zao zipo vyombo vya sheria kwa hatua tofauti wakili wa Serikali Khamis Juma aliwataka watoto hao kutooga Mahamakama na kuona sehemu hio sawa na nyumba zao.
Alisema Mahakama ina wajibu wa kusimamia haki za kila mtu ikiwemo za watoto na ndio maana kesi zinazohusu watoto ziwawekewa mazingira maalumu yenye lengo la kutoa urahisi kwa wahusika kutoa ushahidi.
Sambamba na hayo aliwataka watoto hao kufahamu kuwa wana haki ya kumkataa mtu yoyote kuwemo ndani ya Mahakama pale anapotaka kutoa ushahidi iwapo anahisi kuwepo kwake kunaweza kuzuia kutosema baadhi ya taarifa muhimu za ushahidi ambao utaweza kumtia muhusika mshtakiwa.
Alisema ili Mahakama iweze kumtia hatiani mshtakiwa ni lazima mlalamikaji awe huru kwenye mahakama hio ikiwemo kutoa ushahidi na kueleza tukio zima kama lilivo bila ya kuficha kitu.
Akiendelea kufafanua zaidi Wakili huyo alisema kuhusu kesi za udhalilishaji zinaposikilizwa Mahakamani hakuna idadi maalumu ya mashahidi inayotakiwa badala yake hata mtoto mweyewe aliefanyiwa anaweza kuwa shahidi na Mahakama kupokea ushahidi huo hatima kumtia hatiani aliefanya tukio hilo.
Sambamba na hayo aliwataka watoto hao kutosikiliza maneno ya watu wakiwemo wazazi wao kwenye kutoa ushahidi badala yake wanatakiwa kusema yale waliokutana nayo na sio kuongeza maneno mengine wanayoambiwa wakiwa majumbani mwao.
Akitolea ufafanuzi zaidi alisema kesi za udhalilishaji ili ziweze kupata ufumbuzi ni lazima mtoto alietendewa tukio hio afike Mahakamani kutoa ushahidi hatimae Mahakama iweze kutoa adhabu kwa mhusika.
‘’Kwa mazingira haya ni lazima nyinyi watoto mliofanyiwa udhalilishaji muende Mahakamani tena kwa furaha bila ya woga’’alifafanua zaidi.
Kwa upande wake mkufunzi wa maswala ya saikolojia kutoka chuo cha (ZSH) Asya Saleh Abdullatif aliwataka watoto hao kutokua na uwoga wa kutoa taarifa.
Alisema kikawaida udhalilishaji hufanywa na watu wa karibu na watoto na ndio maana wafanyaji wa matukio hayo huwapa vitisho watoto pale ikitokea watoto kutoa taarifa.
Sambamba na hayo aliwataka watoto hao kutokaa kimya wanapoona viashiria vya udhalilishaji kwa watu wao wa karibu.
‘’Imekua kama kawaida kwenye jamii kuna watu wakiwaita nyinyi mchumba wangu au mke wangu sasa kuanzia leo mtu yoyote yule akiwaambia hivyo msikubali mwambieni mama haraka sana’’aliongezea.
Alisema kikawaida mtukio ya udhalilishaji humkwaza mtu na kumfanya kutokua na furaha siku zote na inawezekana kudumu kwa muda mrefu kwenye akili yake.
Sambamba na hayo alisema matukio hayo yanawafanya watoto na wazazi wao kutoka na furaha na kutumia muda mwingi kufikiria ikiwemo kujaa kwa msongo wa mawazo na kuongezeka kwa wasiwasi.
Aidha aliwataka watoto hao na wazee wao kufahamu kuwa kufanyiwa udhalilishaji sio mwisho wa maisha badala yake wanapaswa kukabiliana na hali hio na kuendeleza harakati nyengine ikiwemo kuwapatia watoto wa elimu.
Baadhi ya watoto hao wamesema wamekua wakihofia kutoa ushahidi kwa kuwa wamekua wakipewa vitisho na wakati mwengine hata kutishiwa kuuwawa.
Walisema baada ya kupatiwa mafunzo hayo ya Tamwa-Zanzibar sasa watasimama kidete kutoa ushahidi Mahakamani kwa kuwa awali walikua hawajui haki zao za msingi kwamba shahidi anahaki ya kuhifadhiwa.
Jumla ya watoto 29 ambao walifanyiwa udhalilishaji kutoka maeneo mbali mbali ya ksiwa cha Unguja wanmejengewa uwezo wa kutoa ushahidi na Tamwa-Zanzibar huku lengo kuu likiwa ni kuwajengea uwezo watoto hao kutoa ushahidi Mahakamani.