**********************************
Na Emmanuel J. Shilatu
Harakati za kampeni za uchaguzi Mkuu zinashika kasi kuelekea upigaji kura Oktoba 28, 2020. Wagombea wapo wengi ila leo nitawaeleza kwanini Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli achaguliwe tena kuwa Rais wa Tanzania.
Kwanini tumpe miaka 5 tena Rais Magufuli?
Sababu 5 za kwanini tumchague Dk. Magufuli awe tena Rais wa Tanzania.
Kwanza; Dkt. Magufuli ndio mgombea pekee kati ya wote mwenye uzoefu wa kiuongozi kitaifa kwa nafasi ya Rais kwani miaka mitano iliyopita alikuwa mgeni lakini sasa anauzoefu wa kutosha, anaijua nchi vilivyo kuliko mgombea yeyote yule. Dkt. John Pombe Magufuli atafanya vizuri zaidi endapo atapewa miaka mingine ya kuwa Rais wa Tanzania kuliko mgombea yeyote yule.
Pili; Haiba yake imebeba uzito na uhalali wa kura yako kwake. Dkt. Magufuli ni kiongozi mwenye sifa zote za uadilifu, uzalendo, uchapa kazi, ufuatiliaji na ucha Mungu. Nyota ya Dkt. Magufuli inang’ara zaidi kutokana na haiba ya matendo na ufanisi wake kiutendaji. Ni uchaguzi Mkuu wa kumpigia kura kiongozi mchapa kazi, mfuatiliaji, muadilifu asiye na makando kando, kura ya turufu hapa inamstahili Rais Magufuli.
Tatu; Kuna kazi kubwa ameianza ya ujenzi wa Taifa anahitaji apewe awamu nyingine ya miaka mitano aweze kuikamilisha. Rais Magufuli ameanzisha ujenzi wa miradi ya kimkakati ya kimaendeleo zaidi ya 50 anayohitaji aongeze muda zaidi aikamilishe tuone matokeo chanya yake. Kumchagua mtu mwingine ni kuharibu mageuzi haya ya kiuchumi.
Nne; Rais Magufuli ameyafanya yasiwezekana yawezekane Tanzania. Mathalani utolewaji wa elimu bure; mapambano ya kweli ya rushwa na ufisadi; maboresho ya utendaji kazi Serikalini; Utoaji wa huduma kwa jamii mijini na vijijini mathalani leo hii umeme upo karibia vijiji vyote, maji mijini na vijijini, huduma bora za afya mpaka maeneo ya vijijini. Kumchagua mwingine nje ya Rais Magufuli ni kujirudisha nyuma miaka 50.
Tano; Rais Magufuli ameendeleza vyema misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kuhakikisha anaondoa matabaka, ukabila, udini na hivyo kuleta umoja, usawa na haki nchini. Ndio maana leo hii hakuna tena ile kauli ya “unanijua Mimi nitakupoteza”, hakuna tena ubabe na unyanyasaji huo kwa wanyonge.
Kwa misingi ya kuchagua kiongozi mwenye sifa zote za kuleta maendeleo, Rais Magufuli ndio suluhisho na matumizi sahihi ya kura yako ya ndio kwake. Mpe 5 tena Rais Magufuli.