Na Masanja Mabula –Pemba.
MAHAKAMA ya Mkoa wa Kaskazini Pemba imemrejesha rumande Hassan Abdalla Hassan anayetumhimuwa kuwashambulia kwa panga mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi –CCM-Wilaya ya Wete pamoja na wanachama wengine wawili.
Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Abdalla Yahya Shamuna , mwendesha mashataka wa serikali Juma Mussa aliiambia mahakama ipange siku nyingine kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashahidi kwa kuwa wakili wa Mtuhumiwa alikuwa nje ya mahakama kikazi.
“Mhe Sheuri lipo kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi , lakini wakili wa mtuhumiwa yuko mahakama Kuu, hivyo naomba kesi hii ipangiwe siku nyengine ambapo mashahidi watafika”alisema.
Alisema “Leo mashahidi hatukuwaleta baada ya kupata taarifa kwamba wakili anayemtetea mtuhumiwa hatafika mahakamani hivyo ikipangwa siku nyingine mashahidi wote watafika”aliongeza.
Aidha Mtuhumiwa huyo aliiomba mahakama impe dhamana , ambi ambalo limepingwa na hakimu wa mahakama hiyo ambaye alisema jukumu la kuomba dhamana litawasilishwa na wakili.
“Hata kama lakini Mhe Hakimu naomba nipatiwe dhamana, naiomba sana mahakama yako ilifikirie hili”alisema mtuhumiwa.
“Ombi hilo litawasilishwa na wakili wako”alisema kwa ufupi.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea tena oktoba 26 ambapo mahakama imeagiza mashahidi waliobakia waweze kuitwa na kusikilizwa.
Mtuhumiwa Hassan Abdalla Hassan anadaiwa kutenda kosa hilo septemba 22 mwaka huu aliwajeruhi watu watatu wakaazi wa shehia ya Kangagani wilaya ya Wete kwa panga wakiwa msikitini wakitekeleza ibada ya swala la asubuhi.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo ni pamoja na Khamis Nyange (65), Bakar Ali Hassan (55) pamoja na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi –CCM Wilaya ya Wete Kombo Hamad Yussuf.