Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mkoani Mara Bw. Alphonce Mlelwa akisisitiza jambo kwa wakazi wa vijiji vya Nyakiswa na Kyankoma Wilayani humo wakati wa hafla ya kutoa hati milki za kimila za kumiliki ardhi 515 kwa wananchi hao iliyofanyika mwishoni mwa wiki, Kulia ni Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe.
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) Dkt. Seraphia Mgembe akieleza faida za hati milki za kimila za kumiliki ardhi zaidi ya 515 zilizotolewa kwa wananchi wilayani Butiama mkoani Mara mwishoni mwa wiki.
Mmoja wa Wananchi wa Wilaya ya Butiama mkoani Mara akipokea hati milki ya kimila ya kumiliki ardhi kutoka kwa Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe wakati wa hafla ya kukabidhi hati hizo mwishoni mwa wiki, baada ya zoezi la urasimishaji mashamba ya wananchi wa vijiji vya Nyakiswa na Kyankoma wilayani humo.
Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini kutoka MKURABITA Bw. Antony Temu akieleza kuhusu utekelezaji wa mpango huo katika wilaya ya Butiama mkoani Mara mwishoni mwa wiki wakati wa hafla ya kukabidhi hati milki za kimila kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Sehemu ya Wananchi wa Wilaya ya Butiama Mkaoni Mara waliopatiwa hati milki za kimila za kumiliki ardhi wakimsikiliza Mratibu wa MKURABITA Dkt. Seraphia Mgembe (Hayupo pichani) wakati wa hafla ya kukabidhi hati hizo mwishoni mwa wiki baada ya zoezi la urasimishaji mashamba ya wananchi hao.
Mmoja wa Wananchi wa wilaya ya Butiama Mkoani Mara, akionesha hati milki ya kimila ya kumiliki ardhi aliyokabidhiwa baada ya zoezi la urasimishaji kufanyika katika vijiji vya Nyakiswa na Kyankoma wilayani humo mwishoni mwa wiki.
(Picha zote na MKURABITA)
…………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum – BUTIAMA
Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania( MKURABITA) umekabidbi zaidi ya hati miliki za kimila 515 kwa wakazi wa vijiji vya Nyakiswa na Kyankoma wilayani Butiama mkoani Mara baada ya MKURABITA kuendesha zoezi la upimaji ardhi katika vijiji hivyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akizungumza kwenye hafla ya kutoa hati hizo hivi karibuni, mwakilishi wa mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Alphonce Mlelwa amesema kuwa, hati hizo zinawasaidia wananchi kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kwamba kati ya hati zilizotolewa, 341 ni za Wakazi wa Kijiji cha Nyakiswa na 174 za Kijiji cha Kyankoma.
“Tumeendelea kushuhudia Serikali ya Awamu ya Tano ikifanya kazi kubwa kuwezesha makundi mbalimbali pamoja na kuwapimia mashamba haya na kuwapatia hati ili wananchi waweze kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi”, alisema
Mlelwa ameeleza kuwa, utekelezaji wa Mpango huo utawawezesha wananchi kujiletea maendeleo endelevu na kuchangia katika kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Mratibu wa MKURABITA, Dkt. Seraphia Mgembe amesema kuwa kati ya hati hizo 135 ni za wanawake huku baadhi ya hati zikimilikiwa kwa panoja kati ya mke na mume, hatua inayolenga kuwakwamua wananchi wote kiuchumi kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
“Serikali imeamua kutoa hati hizi ili kuboresha maisha ya wananchi wake wote hasa wa vijijini kwa kuwa hati hizi ni mojawapo ya kichocheo cha mabadiliko ya kiuchumi hivyo nawaomba wananchi wote kuzitumia katika kujiendeleza kiuchumi sambamba na kuendeleza maeneo yaliyopimwa ili kukuza uchumi wa mtu mmojammoja na maeneo yao kwa ujumla,” Alisisitiza
Dkt. Mgembe amesema mbali na faida za kiuchumi, kutolewa kwa hati hizo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia na hata kumaliza kabisa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikitokea katika baadhi ya maeneo nchini.
Nae, Meneja Urasimishaji Rasilimali Ardhi Vijijini, Bw. Antony Temu amesema, ” Tunaamini kuwa tukiendesha zoezi hili katika vijiji vya mfano,vijiji vilivyobaki vitaona faida na kisha kuishikiniza halmashauri yao kufanya upimaji hatua ambayo ina manufaa makubwa”.
Pamoja hayo, amesema Mpango huo umekuwa ukiwajengea uwezo wananchi kuhusu namna bora kutumia hati hizo na baada ya mafunzo hayo wanaamini kuwa wakazi hao wataongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi kwani zitawawezesha kupata mitaji kwa kutumia hati hizo ambapo changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa wananchi vijijini itakwisha kabisa.
Wakizungumza baada ya kukabidhiwa hati hizo, baadhi ya wanufaika wa mradi huo waliushukuru mpango huo na kusema kuwa hati hizo zitasaidia katika kupata maendeleo endelevu.
Bw. Nelson Msamba amesema wakazi wengi wa vijiji hivyo walikata tamaa baada ya kushindwa kupewa hati hizo kwa wakati baada ya kukamilika kwa upimaji, lakini hivi sasa matumaini yao yamefufuka baada ya kuzipokea na kwamba wanatarajia kuanza kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa uhakika zaidi kwavile uhakika wa kupata mitaji hivi sasa wanao.
MKURABITA tayari imezifikia zaidi ya Halmashauri 50 nchini hapa na kufanya urasimishaji ardhi na biashara ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuwawezesha wananchi..