……………………………………………………………………………………….
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali inataka kuanza ujenzi wa reli ya kimataifa ya kutoka Mtwara – Songea – Mbamba Bay yenye matawi huko Mchuchuma na Liganga.
“Upembuzi yakinifu tayari umeshafanyika na michoro yote iko tayari. Na hii iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ibara ya 59 (d),” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wakazi wa Ndanda, wilayani Masasi katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa mpira wa Njenga.
Ibara ya 59 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM inasema: “Katika miaka mitano ijayo, Chama kitaielekeza Serikali iendelee kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati. Miundombinu hiyo inajumuisha ya reli, viwanja vya ndege na bandari. Pia kuboresha huduma za usafiri wa anga, baharini na kwenye maziwa kwa kununua vyombo vipya vya usafiri na kukarabati vilivyopo ili kuimarisha huduma….”
Kwenye uk.94 ibara ya 59(d) inafafanua kwamba ili kufikia azma hiyo, katika kipindi hicho, miradi itakayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ni pamoja na ujenzi wa reli ya Mtwara – Songea – Mbamba-bay na matawi ya Liganga na Mchuchuma (km. 1,000).
Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Mtwara kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Ndanda, Bw. Cecil Mwambe na mgombea udiwani wa kata ya Njenga, Bi. Ester-Stella Kambanga na wagombea udiwani wengine wa CCM.
Akielezea kuhusu sekta ya maji, Mheshimiwa Majaliwa alisema Serikali ilitoa sh. bilioni 11.2 kwa ajili ya miradi ya maji ya Shaurimoyo, Mkalola, Mpitimbi, Shitingi, Sindano na Lihecha.
Akielezea kuhusu uboreshaji wa barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema ujenzi wa barabara ya Nanganga – Ruangwa kwa kiwango cha lami mkandarasi keshafika site na kazi imeshaanza. Alizitaja barabara nyingine ambazo ziko mbioni kujengwa kuwa ni Masasi – Nachingwea (km.45), Nachingwea – Ruangwa (km. 50) na Nanganga – Masasi (km.45).
Akifafanua kuhusu uboreshaji wa sekta ya elimu, Mheshimiwa Majaliwa alisema sekondari ya Ndanda ni miongoni mwa shule kongwe zinazotupiwa jicho na Serikali na tayari sh. milioni 600 zilishatolewa ili kuanza ukarabati wa bwalo. “Tunataka hii shule irudie kwenye hadhi yake ya zamani,” alisema.
Mheshimiwa Majaliwa alitoa wito kwa wanafunzi wa Ndanda wasome kwa bidii ili watimize ndoto zao na Serikali itaendelea kutoa mikopo ya elimu ya juu. “Wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita wana fursa ya kupata mikopo ya kuendelea na elimu ya juu kwani Serikali hii imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 348.7 na sasa hivi tunatoa shilingi bilioni 464.”
Alisema idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopata mikopo imefikia 130,883 kutoka 98,300 na pia ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini hivi sasa ni 87,813 kutoka 65,064 wa mwaka 2015.