Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Baraza huru na uongozi sikivu wa menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Mohamed Janabi ni mafanikio makubwa ambayo uongozi wa Baraza la nne la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo umejivunia hatua ambayo imetajwa kuimarisha utendaji kazi na kuboresha huduma kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo wakati wa kikao cha baraza hilo kilichofanyika Protea Hotel jijini hapa, Katibu Msaidizi wa TUGHE – JKCI, Joyce Mugala amesema Menejimenti hiyo imekuwa ikipokea hoja zao na kuzifanyia kazi kwa wakati.
“Limekuwa baraza lenye mafanikio, tumeona Mkurugenzi Mtendaji amekuwa akipokea na kufanya yale tunayojadili na kutupa mrejesho kwa wakati, limekuwa baraza sikivu kwani menejimenti imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na wafanyakazi hususan kwa upande wa maslahi,” amesema.
Joyce ameongeza “Kama mnavyojua mgogoro mkubwa wa wafanyakazi ni maslahi na uongozi, lakini tunashukuru Mkurugenzi Mtendaji wetu amekuwa msikivu anatupa kile tunachowasilisha kwa mfano posho kwa wafanyakazi tuliomba kwenye kikao alilichukua na tukapewa,” ametoa mfano.
Joyce ameongeza “Sisi wafanyakazi tunajivunia limekuwa Baraza ‘productive’ maana yale tunayoshauriana na uongozi yanatendewa kazi.
“Vitendea kazi JKCI is perfect hatuna tatizo lolote kwa upande huo, kuanzia mazingira ya ofisi, utendaji ‘theater’ na ‘cathlab’ watu wapo ‘happy’, kutokana na mazingira ya ofisi na vitendea kazi.
“Menejimenti imejali mpaka kufikia hatua ya kuongeza ‘cathlab’ nyingine, tunashukuru pale tunapohitaji kitu, inasikia na kuyafanyia kazi, hii ni maabara ambayo mtaalamu anaweza kuuchunguza moyo ulivyo na kuweza kutibu inapohitajika.
“Furaha ya Watanzania ni pale JKCI inapotoa huduma bora na nzuri kwao, tunakwenda kutoa huduma Bora zaidi,” amesisitiza Joyce.
Naye, Ofisa Ugavi Msaidizi wa JCKI, Rajabu Nasibu amesema kwa upande wa manunuzi kumekuwa na mafanikio Taasisi imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
“Tulipoanza ilikuwa Taasisi changa mwendo wake ulikuwa ukisuasua, hatukuwa na vifaa kama tulivyonavyo sasa, tumepiga hatua, malengo yanaongezeka hata kwa upande wa manunuzi ya vifaa tiba awali watu binafsi ndiyo walikuwa wanavileta nchini sasa hivi Serikali ndiyo inayoagiza na kuleta moja kwa moja nchini,” amesema.
Akizungumza Prof. Janabi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema limekuwa kiunganishi kikubwa kati ya wananchi, wafanyakazi na menejimenti ya Taasisi hiyo.
“Tunajivunia utulivu mkubwa uliopo kwenye Baraza hili, menejimenti inaongoza wafanyakazi 310 na wote wanahitaji kupata huduma wanazostahili ili wananchi wapate huduma ambazo nchi inafikiria kuzitoa kwao,” amesema.