**********************************
NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA VIJIJINI
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani ,Michael Mwakamo amewahakikishia wakazi jimboni hapo ,kushughulikia kero ya mifugo holela ambayo hula mazao mashambani ambapo anaamini itabaki kuwa historia.
Aidha amewataka wakulima kujiandaa katika kilimo na kwamba atahakikisha anasimamia utekelezwaji wa sheria zilizopo, ili kupunguza tatizo hilo.
Mwakamo ametoa kauli hiyo akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Ruvu kwa Dosa Azizi, akiomba kura za kutosha kwa John Magufuli, Ubunge na Udiwani na amewaomba wananchi hao kujitokeza kwa wingi Oktoba 28 kuwachagua wana-CCM.
“Nakumbuka miaka iliyopita mkulima alikuwa analima mpunga, akivuna anapanda mahindi, miwa, maboga sanjali na mboga aina mbalimbali, ambapo kwa miaka ya hivi sasa jambo hilo halipo, sitotumia nguvu nitakwenda kupambana na wanaotakiwa kusimamia sheria zilizopo,” alisema Mwakamo .
Awali wazee wa Kijiji hicho wakiongozwa na Hemed Luwayo na Nuru Mshana waliwafanyia matambiko ya kimira Mwakamo na mgombea udiwani Mwafulilwa, yaliyolenga kuwaombea dua katika safari yao hiyo, ili wachaguliwe .
“Binafsi najisikia vibaya leo hii ninapowaona wazee wetu wakiangaika katika kujitafutia ridhiki kupitia kilimo, ambacho kwa miaka hii imekuwa mtihani mkubwa unaosababishwa na ndugu zetu wafugaji wanaovamia maeneo na mashamba,” alisema Mwakamo.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika mkutano huo kutoka mkoani Rugemalira Rutatina aliwataka wana-Ruvu kwa Dosa kuachana na ushabiki wa kisiasa, badala yake wakichague Chama Cha Mapinduzi chini ya Mgombea wa Urais Dkt. John Magufuli .
Mgombea udiwani Kata ya Mtambani ,Godfrey Mwafulilwa alieleza,katika kijiji cha Ruvu kwa Dosa miaka mitano iliyopita kilikuwa na changamoto ya kukosekana kwa umeme na maji changamoto ambazo zimeshafanyiwa kazi.