Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama mti bora wa kahawa katika shamba la kituo cha utafiti TACRI Mbimba wilaya ya Mbozi jana. Kushoto ni Mtafiti Mkufunzi Dismas Pangaras na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji Mazao Wizara ya Kilimo Beatus Malema. Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kushoto) akisikiliza maelezo ya namna kituo kilivyofanikiwa kuzalisha miche bora ya kahawa toka kwa Meneja wa TACRI Mbimba Isaack Mushi ( wa pili toka kulia) jana .TACRI Mbimba imefanikiwa kusambaza miche bora ya kahawa milioni 11 kwa wakulima 74,565 wa mikoa ya Nyanda za juu kusini katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2020. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akitazama hifadhi ya mahindi katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Songwe. Kushoto ni Kaimu Meneja wa Kanda hiyo Eva Kwavava.NFRA Songwe tayari katika kipindi cha msimu 2020/21 imenunua mahindi tani 9,191 kati ya lengo la tani 30,000 huku ununuzi ukiendelea. Mwonekano wa mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa 6 vyenye uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 20,000 katika kituo cha NFRA Songwe. Mradi huo unatarajia kukamilika Desmba mwaka huu ukigharimu dola za kimarekani milioni 5.2 .Kukamilika kwa mradi huu kutaongea uwezo wa kituo kuhifadhi tani 37,000 za nafaka. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (aliyevaa tai) akisikiliza maelezo ya Mktendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) Dkt.Sophia Kashenge (wa pili toka kushoto) jana alipotembelea shamba la mbegu la ASA Mbozi .Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akimwagilia maji viriba vya miche bora ya kahawa wakati alipokagua uzalishaji miche hiyo kwenye kituo cha utafiti wa kahawa TACRI Mbimba wilaya ya Mbozi jana.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo)
**************************************
Wizara ya Kilimo imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani ya nchi kushirikiana na Wakala wa Mbegu (ASA) kuzalisha mbegu bora nyingi na zenye tija na kuwezesha wakulima kupata kwa gharama nafuu.
Wito huo umetolewa jana (19.10.2020) na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipotembelea na kukagua utendaji kazi wa shamba la Mbegu la ASA Mbozi mkoani Songwe.
“Nakaribisha wawekezaji katiuka uzalishaji mbegu lakini lengo la wizara ni kupata mbegu bora ambazo zitamfikia mkulima kwa gharama nafuu na kwa wakati “alisema Kusaya.
Kusaya ambaye aliambatana kwenye ziara hiyo pamoja na makampuni yanayojihusisha na uzalishaji mbegu pamoja na ASA ikiwemo Jeshi la Kujenga Taifa aliwataka kuendelea kutumia ardhi kubwa iliyopo kuzalisha mbegu bora zinazohitajika na wakulima wa Tanzania na kupunguza utegemezi wa nje.
“Natoa rai kwa Jeshi la KLujenga Taifa njooni hapa Mbozi mshirikiane na wakala wetu ASA mzalishe mbegu bora ili ushirikano wetu usaidie Taifa kuwa na mbegu bora zilizotafitiwa na watanzania wenyewe badala ya mbegu za kutoka nje ya nchi” alisisitiza Kusaya.
Akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji mbegu za mazao nchini, Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge alisema wakala huo unayo mashamba 10 yanayozalisha mbegu takribani asilimia 21 hdi 25 inayotumika nchini.
Dkt. Sophia aliongeza kusema katika mwaka 2020/21 wakala kwa ushirikiano na makampuni binafsi na taasisi za umma umeweza kuzalisha mbegu mbalimbali za mazao tani 5,600
Kuhusu uzalishaji wa mbegu bora za michikichi aina ya Tenera zenye kutoa mavuno mengi,Dkt. Sophia alisema ASA tayari imefanikiwa kuzalisha miche 342,000 katikam vituo vyake vitatu ambayo itagawiwa kwa wakulima wa Kigoma,Morogoro na Mbozi.
Katibu Mkuu Kilimo alipongeza ASA kwa kuzalisha miche bora ya michikichi 42,000 katika shamba lake la Mbozi hali itakayosaidia kuongeza wigo wa uzalishaji michikichi kama livyoagizwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Kusaya alisema Tanzania kwa sasa inatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 443 kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi hivyo lengo la seriklai kuhamasisha kilimo cha michikichi ili nchi ijitosheleze kwa mafuta.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo alitembelea Kituo cha Utafiti wa kahawa (TACRI) Mbimba wilayani Mbozi na kufahamishwa kuwa kituo hicho kimefanikiwa kuzalisha na kusambaza miche bora ya kahawa milioni 11.2 kwa wakulima wa mikoa ya Songwe, Mbeya,Rukwa na Katavi katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2020.
Akitoa taarifa ya kituo hicho Meneja wa TACRI Mbimba Isaack Mushi aliongeza kusema kituo kimefanikiwa pia kuwafikia wakulima 74,565 katika wilaya 10 za Nyanda za Juu Kusini na kuwapa elimu ya kilimo bora cha kahawa.
“Msimu wa 2020/21 tunatarajia kuzalisha na kusambaza miche bora ya kahawa milioni 4.5 kwa wakulima hali itakayokuza uzalishaji kahawa” alisema Mushi.
Kuhusu takwimu za unywaji kahawa Mushi alisema watanzania wanakunywa kahawa asilimia 7 tu ya kahawa yote inayozalishwa nchini hali inayopunguza upatikanaji wa soko.
Katibu Mkuu Kusaya alitoa agizo kwa watafiti wa zao la kahawa kuongeza bidii ya kuwezesha miche mingi ya kahawa iwafikie wakulima na kukuza uzalishaji wa zao hilo ambalo linaingiza fedha nyingi nchini.
Kusaya alisisitiza umuhimu wa mbegu bora za kahawa na kusema” tunahitaji mbegu bora nyingi himilivu kwa magonjwa na zenye kuongeza tija kwa mkulima katika mazingira yake “na kuongeza kuwa watafiti wanalo jukumu la kuwezesha ubora wa kahawa inayozalishwa Tanzania kuwa na soko la uhakika.
Katika hatua nyingine akiwa mkoani Songwe, Kusaya alikagua mwenendo wa ununuzi wa mahindi katika kituo cha wakala wa Taifa wa Chakula (NFRA) Songwe na kuelezwa kuwa tayari tani 9,191 za mahindi kati ya lengo la tani 30,000 msimu wa 2020/21 zimenunuliwa toka kwa wakulima kwa bei ya wastani ya shilingi 550.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Meneja wa NFRA kanda ya Songwe Eva Kwavava ilisema kituo hicho kina uwezo wa kuhifadhi tani 17,000 za nafaka na mpaka mwezi Octoba mwaka huu kina nafaka tani 10,483 zilizohifadhiwa kwenye maghala yake.
Kusaya alikagua pia mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa 6 vyenye uwezo wa tani 20,000 vinavyojengwa na mkandarasi M/S Feerum S.A ya Poland na kusimamiwa na Wakala wa Majengo (TBA) ambayo vinatarajia kukamilika Desemba 2020 kwa gharama dola za kimarekani milioni 5.2.
Wakala wa Taifa wa Hifadhi wa Chakula katika msimu unaoendelea wa ununuzi tayari umenunua tani 110,000 kati ya lengo la tani 300,000 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 15 zilizotolewa na serikali katika kanda zake nane nchini.
Katibu Mkuu Kusaya leo anaendelea na ziara yake mkoani Rukwa kwa kutembelea taasisi chini ya wizara na kuzungumza na watumishi wa sekta hiyo.