Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (katikati) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI ) Uyole Dkt. Tulole Bucheyeke (kushoto) jana alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua utekelezaji wa agizo lake la kusitishwa kwa shughuli za taasisi ya STAWISHA ndani ya eneo la umma ambapo limetekelezwa. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji Mazao Wizara ya Kilimo Beatus Malema.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akizungumza na Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI ) Uyole cha Mbeya Dkt. Tulole Bucheyeke (kushoto) jana alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua utekelezaji wa agizo lake la kusitishwa kwa shughuli za taasisi ya STAWISHA ndani ya eneo la eneo la serikali baada ya kukiuka mkataba wa makubaliano.
Shamba la ngano likisubiri kuvunwa ndani ya eneo la TARI Uyole leo wakati Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo lake la kusitishwa kwa shughuli za taasisi ya Stawisha kwa kukiuka mkataba wa makubaliano alilotoa tarehe 21 Julai mwaka huu .TARI Uyole imeelekezwa kuvuna mazao hayo ikiwemo viazi na kuvitumia kwa manufaa ya umma.
………………………………………………………………………………..
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ameridhishwa na kitendo cha taasisi ya STAWISHA ya Mbeya kutekeleza agizo la serikali la kusitisha shughuli zake ndani ya eneo la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Uyole.
Akizungumza leo jijini Mbeya Katibu Mkuu Kusaya alipofanya ziara ya kushtukiza ndani eneo la Uyole zilipokuwa ofisi za Taasisi ya Kuendeleza Zao la Viazi Mviringo (STAWISHA) na kukuta walinzi pekee huku mazao ya ngano na viazi vikiwa vimekomaa mashambani.
Katibu Mkuu huyo wa Kilimo alisema agizo lake la kusitisha shughuli za taasisi ya Stawisha alilitoa tarehe 21 Julai mwaka huu jijini Dodoma lilitokana na kukiukwa kwa mkataba wa makubaliano kulikofanywa na Stawisha.
“Mali hii mnayoiona humu ndani ikiwemo mazao ya ngano na viazi mviringo ni ya watanzania, naagiza TARI Uyole mchukue hatua za kuvuna, kwa kuwa Stawisha hawapo tena hadi pale nitakapotoa maelekezo mengine” alisisitiza Kusaya.
Katibu Mkuu huyo alitembelea eneo hilo na kujionea mashamba ya ngano ,viazi mviringo, ghala la mahindi na baadhi ya mitambo ya kilimo vilivyoachwa na taasisi ya Stawisha kufuatia kukiuka mkataba wa mashirikiano uliosainiwa kati ya wizara ya kilimo na ubalozi wa Uholanzi mwaka 2018.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Uyole Dkt. Tulole Bucheyeke alisema atatekeleza agizo la Katibu Mkuu la kuvuna mazao yote ndani ya eneo lililokuwa la Stawisha.
Dkt. Bucheyeke alisema tayari uongozi wa TARI umefanikiwa kubadilisha kibali cha ujenzi wa majengo ya ofisi za Stawisha kwa kuwa hilo ni eneo la serikali chini ya TARI lakini Stawisha walijimilikisha kinyume cha utaratibu.
“Tayari kibali cha ujenzi kimebadilishwa kuwa cha TARI na siyo Stawisha tena kama alivyoagiza Katibu Mkuu Kilimo tarehe 21 Julai mwaka huu kule Dodoma” alisema Bucheyeke
Aidha Kusaya ameutaka uongozi wa TARI Uyole ufanye kazi ya kusafisha eneo hilo na kutunza mazao yaliyomo ndani ya maghala ikiwemo kupiga dawa ili yasiharibike hadi pale Ubalozi wa Uholanzi utakapokamilisha majadiliano na serikali kuhusu uhalali wa taasisi ya Stawisha.
Serikali ilifikia hatua za kusitisha shughuli za Stawisha baada ya kubaini kukiuka mkataba wa makubaliano uliotaka taasisi hiyo kufanya kazi za utafiti wenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa zao la viazi mviringo lakini watendaji wake wakaamua kufanya biashara ya mazao bila kibali cha serikali.
Mwisho.
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo
MBEYA
18.10.2020