Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe katikati akikata utepe kuashiria kukizindua rasmi kivuko kipya cha MV.UKARA II HAPA KAZI TU katika sherehe zilizofanyika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza leo. Kivuko cha MV. UKARA kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 na kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 sawa na tani 300.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe akibonyeza kitufe na kufungua pazia kuonyesha kuzindua rasmi kivuko kipya cha MV.UKARA II HAPA KAZI TU katika sherehe zilizofanyika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza leo. Kivuko cha MV. UKARA kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 na kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 sawa na tani 300.
Wananchi wa visiwa vya Ukara, Bugorola na maeneo ya jirani wakisubiri kuingia katika kivuko kipya cha MV.UKARA II HAPA KAZI TU mara baada ya kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe katika sherehe zilizofanyika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza leo. Kivuko cha MV. UKARA kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 na kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 sawa na tani 300.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe akishuka kutoka kwenye kivuko kivuko kipya cha MV.UKARA II HAPA KAZI TU mara baada ya kukizindua rasmi mapema leo katika sherehe zilizofanyika katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza. Kivuko cha MV. UKARA kimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 na kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 sawa na tani 300. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Saleh Songoro na wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle, Katibu Mkuu wa Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga, viongozi wa dini mbalimbali na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa mkoa wa Mwanza wakiwaombea marehemu wa ajali ya kivuko cha MV. NYERERE kilichozama mwaka 2018 katika mnara wa kumbukumbu ilipozikwa miili ya baadhi ya wahanga wa ajali hiyo.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA) UKEREWE MWANZA
……………………………………………………………………..
Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) leo imefanikiwa kurejesha faraja ya wakazi wa visiwa vya Bugorola na Ukara baada ya kuzindua kivuko kipya kilichogharimu shilingi bilioni 4.2, MV.UKARA II (HAPA KAZI TU). Kivuko hicho kipya ambacho kimejengwa na mkandarasi mzawa Songoro Marine Transport ya jijini Mwanza kina uwezo wa kubeba abiria 300 na magari 10 ambazo ni sawa na tani 100.
Akizungumza na wananchi wa visiwa hivyo mapema leo mara baada ya kuzindua kivuko hicho, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe alisema ujenzi wa kivuko cha MV.UKARA ni agizo lililotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli baada ya ajali ya MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 Septemba, 2018, ambapo kupitia kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, aliagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufanya ununuzi wa Kivuko kipya na kikubwa kwa ajili ya Wananchi wa Ukara na Bugolora.
‘’Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa vivuko vyote nchini vinakuwa vya uhakika na salama kwa matumizi ya wananchi kwa kuvikarabati na kununua vipya pale vinapohitajika kadiri uwezo wa Bajeti ya Serikali unavyoruhusu’’. Alisema Mhandisi Kamwelwe ambapo aliongeza kuwa katika kutekeleza hayo, Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) inaendelea na miradi ya ujenzi wa vivuko vipya vya Chato – Nkome/Mharamba na Nyamisati – Mafia ambavyo navyo vinatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Aidha Mhe. Kamwelwe alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha usimamizi wa uendeshaji wa vyombo vya majini ili kuepusha matukio ya ajali ambapo katika kutekeleza azma hiyo wameipa majukumu TASAC kuhakikisha inaweka maafisa wasimamizi katika maeneo yote ya usafiri wa majini na kuendelea kutoa mafunzo kwa wamiliki na waendesha vyombo vya usafiri majini ikiwemo TEMESA ili kuwaongezea ufahamu juu ya umuhimu wa kuzingatia taratibu na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa vyombo hivyo.
‘’kwasababu kinakwenda sio zaidi ya saa moja, Mtendaji Mkuu nakuagiza urekebishe ratiba ili wana Ukara wawe karibu na Mwanza ili wawahi meli zakwenda na kurudi Mwanza.’’ Alisema Mhe. Waziri.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya Ujenzi Arch. Elius Mwakalinga, akizungumza katika tukio hilo, alisema kuwa Ujenzi kivuko cha MV.UKARA II ulianza mwezi Februari, 2019 lakini umechelewa kukamilika kutokana na vifaa vilivyokuwa vimeagizwa kutoka nje ya nchi kuzuiwa kutokana na ugonjwa wa COVID – 19. Baada ya vifaa kuwasili Mkandarasi alifanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi wa kivuko ambapo alimmpongeza kwa hatua hiyo.
‘’Mhe. Mgeni rasmi kivuko hiki amekijenga kwa shilingi bilioni 4.2, wakati wakandarasi wa nje walikuwa wanataka wakijenge kwa shilingi bilioni 22, sasa unaweza kuona kwanini unaweza k huyu mkandarasi ni mzalendo kweli.’’ Alimaliza Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu aliongeza kuwa Serikali ina dhamira ya kutaka kutoa huduma iliyo bora yenye kukuza uchumi wa nchi ya Tanzania na ndiyo maana imekuwa ikitoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo.
‘’Serikali katika mwaka wa fedha 2019/20 imetoa jumla ya Shilingi Billioni 12,245,214,800.00 kwa ajili ya miradi ya vivuko na maegesho ambayo inatekelezwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA).’’ Alisema Arch Mwakalinga ambapo aliongeza kuwa Fedha hizi zinatokana na Mfuko Mkuu wa Serikali na Mfuko wa Barabara.
Awali akisoma tarifa ya ujenzi wa kivuko cha MV.UKARA II, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle alisema kivuko hicho kina urefu wa mita 42.00 na upana wa mita 10 na kimefungwa injini mbili aina ya DOOSAN INFRACORE ambazo uwezo wake ni “Horse Power” (HP) 360 kila moja na kinabeba abiria wengi zaidi tofauti na kivuko cha zamani (MV Nyerere) ambacho kilikuwa na uwezo wa kubeba tani 25 yaani abiria 101, magari 4 na mizigo.
Mhandisi Maselle aliongeza kuwa kivuko hicho kinaendeshwa na mifumo mitatu ya usukani (steering) moja kati ya hizo ni Hydraullics, Electro-Hydraullic na Emergency. utakuwa ni wa dharura (emergency steering system). Pia vivuko hivi kimejengwa kwa kutumia mabati maalumu (grade A marine plate) yanayotumika kujengea vyombo vya usafiri wa majini.
Vilevile Mtendaji Mkuu aliongeza kuwa TEMESA inatekeleza miradi mingine ya ujenzi wa vivuko vipya vitatu ambayo ni ujenzi wa kivuko kipya cha Chato – Nkome/Muharamba ambacho ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 95, kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100, yaani abiria 200, magari madogo 10 na mizigo na kinatarajiwa kukamilika tarehe 25 Oktoba, 2020 na kitagharimu shilingi za Kitanzania bilion 3.12, ujenzi wa kivuko kipya cha Nyamisati – Mafia ambacho umefikia zaidi ya asilimia 95. Kivuko hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100, yaani abiria 200, magari madogo 6 na mizigo na kinatarajia kukamilika mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2020 na kitagharimu shilingi za Kitanzania billion 5.3.
Alisisitiza kuwa miradi hii yote inafanywa na kampuni ya M/S SONGORO MARINE TRANSPORT LTD. BOATYARD na fedha zote zimetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kukamilika kwa ujenzi wa kivuko cha MV.UKARA HAPA KAZI TU kunafanya idadi ya vivuko mpaka sasa kufikia 31 nchi nzima.
MWISHO