Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya UVCCM Taifa, Tabia Mwita akimnadi mgombea udiwani Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia kwenye uzinduzi wa kampeni katika uwanja wa CCM Kata ya Endiamtu.
Mgombea udiwani kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia Agwiso akiwapungia mikono wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani katika maandamano ya kuelekea kwenye uzinduzi wa kampeni ya CCM Kata ya Endiamtu.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya UVCCM Taifa, Tabia Mwita akiwanadi mgombea ubunge jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka (kulia) na udiwani Kata ya Endiamtu Lucas Chimbason Zacharia Agwiso (katikati) kwenye uwanja wa CCM Kata ya Endiamtu.
*****************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
MGOMBEA udiwani wa Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwa tiketi ya CCM, Lucas Chimbason Zacharia amewaomba wananchi wa eneo hilo kumkopesha kura ili awalipe maendeleo.
Zacharia ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa kampeni yake ya kugombea udiwani katika kata ya Endiamtu ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya UVCCM Taifa, Tabia Mwita.
Amesema mwaka 2010 hadi 2015 alikuwa diwani wa eneo hilo na maendeleo mengi waliyaona ila mwaka 2015 wakafanya makosa kwa kuchagua diwani wa upinzani mwaka huu wasirudie tena.
“Mimi ni mtu wa maendeleo nitawasemea kule halmashauri wanawake, vijana na walemavu mpate mikopo na kufanikisha changamoto nyingine za elimu, afya na maji,” amesema Lucas.
Amesema kituo cha afya Mirerani kipo kwenye mchakato wa kuwa hospitali teule kwani kinahudumia watu wengi na atapambania eneo huru la biashara EPZA ianze ujenzi na shughuli zifanyike humo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa jumuiya ya UVCCM Taifa,Tabia Mwita amesema ilani ya CCM imezungumzia uboreshaji wa wachimbaji wadogo wa madini hivyo wananchi wakichague chama hicho.
“Endapo nitasahau kuzifikisha changamoto zenu zinazowakabili kwenye madini, Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Manyara, Mosses Komba atanikumbusha ila nawaahidi siwezi kuzisahau,” amesema Mwita.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema mgombea urais atakayeweza kutatua changamoto zilizopo kwenye lango la ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ni mgombea wa CCM, John Magufuli pekee.
Ole Sendeka amesema Dk Magufuli anaweza kutatua changamoto hizo akifikishiwa na mbunge wa CCM kwa kujenga hoja na siyo kupayuka mitaani.
Mbunge mteule wa vijana, Asia Halamga amesema kupitia madini ya Tanzanite vijana wengi wamefaidika nayo.
Mbunge mteule viti maalum mkoani Manyara, Martha Umbullah amesema mgombea urais wa CCM amewaletea maendeleo mengi wananchi wa mji mdogo wa Mirerani hivyo wampe kura za ndiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoani Manyara, Mosses Komba amewaomba wananchi wa eneo hilo kuwachagua wagombea nafasi ya urais, ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM.
Mwenyekiti wa chipukizi Mkoani Manyara, Abubakari Zimbwe amewaomba wananchi wa Simanjiro kuhakikisha wanapiga kura kwa kulenga mafiga matatu ya CCM kwa urais, ubunge na udiwani.