Na Judith Mhina- Maelezo
Nani asiyejua Baba wa Taifa, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mpigania Uhuru wa Serikali ya Tanganyika kutoka mikononi mwa wakoloni wa Uingereza mwaka 1961 na Tanganyika kupata uhuru kamili kutoka mikononi mwa Gavana wa mwisho wa Tanganyika Sir Richard Turnbull.
Mwalimu mwaka 1964, wewe na Shekhe Abeid Amani Karume kwa niaba ya wananchi wenu yaani Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mliamua kufanya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuzaliwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha makubaliano maalum ya kuwa na maeneo ya muungano kama vile Ulinzi na Usalama ili Muungano wetu kuwa imara zaidi.
Hukuishia hapo mwaka 1964, Mwalimu aliunda rasmi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kumteua Mkuu wa Majeshi wa Ulinzi na Usalama Mtanzania na kumtunuku cheo cha Meja Generali Mirisho Sarakikya ambaye alikuwa ni miongoni mwa maafisa wa Jeshi wa hali ya juu katika kipindi hicho na msaidizi wake kutoka Zanzibar aliteuliwa Brigedia Yusuf Himid.
Moja ya kazi za awali ambazo Mwalimu ulifanya ni kuhakikisha anawaunganisha Watanzania kwa kujenga umoja wa Taifa kwa kutumia lugha ya Kiswahili, ambapo shule zote nchini kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, pamoja na shughuli za Serikali zikaanza kufanyika kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili. Aidha, uliondoa dhana ya ubaguzi iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni ukahakikisha unapiga vita Ukabila, Udini, Ubaguzi wa rangi ili Watanzania wote kujiona wamoja kama ndugu wa familia moja.
Dhamira yako ilikusukuma kufanya kazi ya kuhimiza umoja na mshikamano wa kikanda, Afrika na dunia kwa ujumla kwa kuanzisha Jumuia mbalimbali na kushiriki kama kiongozi wa umoja Barani Afrika kupitia Umoja wa Nchi Huru za Afrika(OAU) na baadaye Umoja wa Afrika (AU).
Hakika tunakukumbuka Mwalimu. ulituondolea pengo kubwa kati ya walichonacho na wasionacho ambapo ulijua litaleta tatizo katika nchi, hivyo ulihakikisha Watanzania kwa asilimia kubwa hawapishani sana katika kipato. Ili kuhimili hili ulidhibiti rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali za Umma kwa kuhakikisha kinachopatikana katika Taifa kinatumiwa na Watanzania wote katika kujenga Taifa huru lenye kujitawala na kujiamini.
Nani asiyejua kuwa wewe Mwalimu uliwafikiria zaidi wanyonge na masikini wa Tanzania kwa kuhakikisha katika Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano unaanzisha Kampeni mbalimbali na kuziingiza katika utekelezaji ambao uliwashirikisha moja kwa moja wananchi. Mfano Siasa ni Kilimo, Ukulima wa Kisasa, Chakula Bora, Elimu ya Watu Wazima, Mtu ni Afya, ili kuondoa maadui watatu wakubwa Maradhi, Ujinga na Umasikini.
Ulitambua kuwa nchi yetu ni changa inayopigana usiku na mchana kupunguza kama sio kuondoa kabisa umasikini, Mwalimu ulikuja na sera ya Elimu Bure, kuanzia shule za Msingi hadi Chuo Kikuu ili kutoa fursa kwa watoto wote wa Tanzania kupata elimu ambayo itawakomboa katika Ujinga, Umasikini na Maradhi
Bado tunatafakari na kujiuliza ulifanikiwa kujenga viwanda vingi takriban 414 na kuanzisha Mashirika ya Umma kama Kiwanda cha Viatu –BORA Kiwanda cha Bia Tanzania -TBL, Kiwanda cha Sigara ,-TCC, Shirika la Usagaji la Taifa – NMC, Tanzania Shipping Company Limited-TACOSHILI, Tanzania Fisheries Company-TAFICO. Pia, Taasisi za fedha kama Benki ya Taifa ya Biashara, (National Bank of Commerce), Community Rural Development Bank-CRDB, Tanzania Postal Bank-TPB. Mashirika yote hayo yalilenga kutumia rasilimali zitokanazo na kazi za wakulima, wafugaji na wavuvi ambao asilimia kubwa ya Watanzania wanajishughulisha na sekta hizo ili kuongeza thamani ya mazao yao na matumizi ya chakula kwa Watanzania, kuhifadhi fedha zao, kujipatia kipato kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Kamwe hatuwezi kusahau Mwalimu wewe ndiye uliyeshauri na kutoa pendekezo la kupigania serikali ya Jamhuri ya Watu wa China (The People Republic of China) kujiunga na Umoja wa Mataifa ( United Nation), kwenye miaka ya 1970 wakati huo Jamhuri ya Watu wa China Bara ilikuwa na jumla ya watu milioni 800 na kisiwa cha Taiwan ambacho kilikuwa kinawakilisha China katika UN kilikuwa na jumla ya watu milioni 18. Mwalimu ulimuagiza Balozi wetu wakati huo katika Umoja wa Mataifa Dkt. Salim Ahmed Salim kuwa ahakikishe China inaingizwa UN na kuwa mwanachama wa umoja huo.
Baba wa Taifa wewe na wasaidizi wako waaminifu kama Dkt . Salim Ahmed Salim ulitoa pendekezo hilo kwenye Umoja wa Mataifa na kuwauliza kwa nini Taiwan ikiwa na idadi ndogo ya watu inaiwakilisha China Bara kwenye Umoja wa Mataifa badala ya China Bara kuiwakilisha Taiwan yenye idadi ndogo ya watu na eneo dogo la kijiografia, UN walikaa kikao na kujadili mapendekezo hayo ya Serikali ya Tanzania juu ya Jamhuri ya Watu wa China kuwa miongoni mwa nchi wawakilishi katika Umoja huo na kura zilipigwa ili kumpata mwakilishi halali kati ya China Bara na Taiwan baada ya kura China Bara ilishinda hapo ndipo Tanzania ilipoanza kujulikana Kimataifa.
Wapo wanaobeza juhudi zako Mwalimu sisi Watanzania tunawalaani, wakumbuke mchango wako katika kupigania uhuru Mwalimu umevunja rekodi ya viongozi wa nchi huru za Afrika kwa kuzisaidia nchi nyingi za Afrika kuweza kupigania uhuru wao, kama vile Afrika ya Kusini, Angola, Zimbabwe, Namibia, Msumbiji na kuwasaidia wananchi wa Uganda kumng’oa nduli Iddi Amin Dadah aliyewatawala Waganda kimabavu, kuwauwa wananchi wengi wasiokuwa na hatia pamoja na wasomi na viongozi wa dini kama alivyoamuru kuuliwaa kwa Askofu Luwumu na watu wengi mashuhuri nchini Uganda.
Pia, wanajua kuwa Nyerere ndiye aliyeongoza nchi nyingi za Afrika kupambana na vibaraka wa waliokuwa wanataka kusimikwa na mabeberu katika visiwa cha vya Ushelisheli na Comoro. Mwalimu alihakikisha Jeshi la Wananchi la Tanzania –JWTZ linapambana na vibaraka hao na kuwang’oa na kuwarudisha madarakani viongozi waliochaguliwa na wananchi.
Mchango wako Mwalimu umetukuka kwani uliongoza mapambano ya kuzikomboa nchi zote za Kusini mwa Afrika ikiwemo Msumbiji, Angola, Afrika ya Kusini, Southern Rhodesia- Zimbabwe, Namibia. Wakati wa Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika Nelson Mandela alkuwa kwenye gereza la Robin highlands ambako alikuwa anatumikia kifungo cha maisha chini ya Utawala wa Makaburu. Mwalimu alipambana kwa kutumia kila aina ya mbinu za kutoa hoja makini, kijeshi na kisiasa, hatimaye Mandela akaachiwa huru 1990.
Viongozi hao bado wanakumbuka kwani uliiwahifadhi wapigania uhuru na kuwapa majina na uraia wa Tanzania ili waweze kupambana kwa nguvu zote na mabeberu walowezi, Makaburu na waliokalia kinyume ardhi ya wazalendo na wananchi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Pia, uliwahamasisha Watanzania walichangia misaada ya hali na mali kwa wapigiania uhuru.
Uadilifu wako uliotukuka Mwalimu, wewe ni kiongozi mudilifu wa mali za umma, hukuwa na tamaa ya kuchota kwa kujilimbikizia na kuzifuja rasilimali za Taifa. Pia, hukuwa mfujaji wa fedha za umma wala za Serikali na uliishi maisha ya kawaida kwa muda wote wa miaka 24 uliokaa Ikulu kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakika tumekosa kuuona ucheshi wako na uliipenda kuwasikiliza wananchi wote waliokuwa wasomi na hata wasiokuwa wasomi. Pia ulipenda sana kuongea na wazee waliokuzidi umri ili kupata busara zao na kuelewa nini wanachikitaka ili kupata mwelekeo wa Taifa na uongozi na pale unapogundua kuwa kuna kasoro ulirekebisha haraka.
Huruma yako Mwalimu Nyerere nani asiyeijua kiasi kwamba uliweza kuwasamehe watu ambao walitaka kupindua Serikali yako na kutaka kumwaga damu ya Watanzania wasiokuwa na hatia. Matukio hayo yalitokea miaka ya 1971 na mwaka 1974, ambapo wahaini hao waliwekwa ndani kwa muda na kutumikia kifungo cha ndani na wengne cha nje na mwishowe kupata msamaha wa Rais rnpaka sasa wapo.
Jaribio hilo kisheria hukumu yake ilikuwa kifungo cha maisha au kunyongwa hadi kufa au kupigwa risasi hadharani.
Kifo chake Mwalimu kilikuwa uthibitisho kuwa Mwalimu alikuwa kipenzi cha Watanzania wote na dunia kwa ujumla. Kwani nchi yetu ilionesha kuzizima na baadhi ya mataifa ya nchi za Afrika kama Afrika ya Kusini, Namibia, Zimbabwe, Angola, Msumbiji, Rwanda, Kongo DRC, Uganda, Burundi, Zambia na wengine ambao hawakutajwa walihudhuria mazishi yake kitaifa.
Aidha Mataifa ya Ulaya, Asia na Marekani iliyowakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje Mheshimiwa Madeline Albright kwa kuwa Tanzania hususan Mwalimu ni muhimu katika kuleta utulivu na amani Barani Afrika alihudhuria mazishi yake na kuonyesha kusititishwa na kusononeshwa na msiba huo. Pia Mwalimu alikuwa tayari kukabali jambo lolote la kupambana na mabeberu ili kuleta utulivu wa nchi na maridhiano. PUMZIKA KWA AMANI MWALIMU
MWISHO