.
Na Dotto Mwaibale
WANAMUZIKI nchini wametakiwa kuhamasisha amani katika uchaguzi mkuu na kwenda kupiga kura ifikapo Oktoba 28 ili kuwachagua viongozi wanao wataka.
Ombi hilo linetolewa na Rais mpya wa Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO) Erick Kisanga wakati akizungunza na waandishi wa habari jijini Arusha.
“Nina wahimiza wanamuziki wote hapa nchini wajitokeze kupiga kura kwa Rais, wabunge pamoja na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwezi huu” alisema.
Kisanga amewaomba watanzania kuombea uchaguzi huo ili Mungu atujalie kuwapata viongozi watakaoliongoza vema Taifa letu la Tanzania na kuwaomba wanamuziki kuendelea kutunga na kuimba nyimbo za kuhamasisha amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Wanamuziki ni watu muhimu kupeleka ujumbe haraka kwa wananchi kupitia nyimbo zao hivyo niwaombe katika hizi siku chache zilizosalia wahamasishe kujitokeza kupiga kura na kulinda amani ya nchi.
Kisanga alisema kila mwanamuziki mwenye sifa ya kupiga kura ajitokeze na kadi yake ya kupigia kura katika kituo alichojiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi na ya kikatiba.
Aidha Kisanga alilisitiza umuhimi wa kila mtanzania kuzingatia misingi ya amani na utulivu wakati mchakato huo ukiendelea, ikiwemo kufika mapema kituoni kupiga kura na kuondoka kuelekea kwenye majukumu mengine kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kuepusha madhara au viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza.