Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt.Hassan Abbasi, amewaongoza Wanahabari na Wasanii kutembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) ambapo kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kipo mbioni kukamilika.
Akizuingumza katika Ziara hiyo, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali itaendelea kupeleka makundi mbalimbali ili wakajionee mradi huo mkubwa ambao unatekelezwa wa fedha za ndani shilingi trilioni 7, ukifuatiwa na mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JHPP), ambao unatekelezwa kwa shilingi trilioni 6.5.
“Ziara hii ina lengo moja tu, kwanza ni kuwaonesha Wanahabari na Wasanii wetu mradi huu mkubwa kwa nchi yetu, ni kundi la kwanza kuja kutembelea na kujionea utekelezaji wa mradi wa Reli ya kisasa (SGR) ambao umefikia asilimia 95 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro. Kwa hiyo Wanahabari na Wasanii kama raia wamepata hali halisi ya nini Serikali inafanya”, ameeleza Dkt.Abbasi.
Aidha, Dkt. Abbasi alisema kuwa Serikali inatekeleza miradi mingi katika kila sehemu kama ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara nyingi, ujenzi wa hospitali za Wilaya 67, ujenzi wa meli katika kila Maziwa pamoja na ile meli kubwa katika Ziwa Victoria, ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo wanahabari na Wasanii wamepa fursa mzuri wa kutembelea nakujionea.
Dkt. Abbasi aliongeza kuwa mradi huo ambao ni moja ya miradi mikubwa unafanyiwa majaribio kwa treni ya kihandishi ambayo Wanahabari na Wasanii leo Oktoba 16, 2020 walipataa nafasi ya kupanda na kujionea utekelezaji wa mradi huo wenye thamani kubwa ya fedha.
“Hii ni treni ya Kihandisi ambayo inatumiwa na wahandishi kusafirisha vifaa na wafanyakazi, bado itakuja treni yenyewe yenye mabehewa ya kisasa, vituo vya kisasa na treni ya kisasa ya umeme ambayo itakuwa na kasi kubwa ya kilimeta 160 kwa saa itakuwa ya pili barani Afrika kuwa na kasi ya namna hii tukifungana na Afrika kusini na Ethiopia ikitanguliwa na reli ya kisasa ya Morroco yenye kasi ya kilimeta 300 kwa saa”, amesema Dkt. Abbasi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania, Masanja Kadogosa amesema kuwa ujenzi wa Reli hiyo ya kisasa kupita zote Uganda vizuri na kwamba watanzania wataanza kutumia miundombinu hiyo ya kisasa hivi karibuni.
“Ujenzi wa Mradi huu mkubwa wa SGR ulikuwa unazungumzwa tu, lakini sasa hivi siyo jambo la kuzungumza tena mmejionea na mmepanda na kuona jinsi inavyofanya kazi japo ni treni ya kihandisi, mradi huu uko vizuri sana kitu hiki Mhe. Rais Magufuli aliahidi na ametekeleza kwa awamu hii ya kwanza ambayo sasa hivi umefikia asilimia 95 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
Kadogosa aliwaomba wananchi kuamini kuwa masuala hayo ya miradi mikubwa kama Taifa, yanaweza kutekelezeka kwa kodi zao na kusimamiwa na watanzania wenyewe na kwamba ina manufaa kwa nchi.