Wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiendelea na shughuli za kutafuta madini hayo mgodini.
***********************************
Na Joseph Lyimo, Manyara
Mwanzoni mwa mwaka huu, Tanzania ilikumbwa na changamoto ya maambukizi ya virusi vya corona na kusababisha hofu kwenye baadhi ya maeneo mbalimbali hapa nchini.
Machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ni miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wake waliendelea kufanya kazi zao za shughuli za uchimbaji bila kuathirika na maambukizi ya virusi hivyo vya corona.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani, Ezekiel John anasema wanamshukuru Mungu kwenye machimbo hayo hakukutokea na tatizo la janga la maambukizi ya virusi vya corona.
John anasema wachimbaji madini walikuwa na hofu ya kufungwa kwa machimbo hayo lakini wanashukuru serikali haikufanya hivyo.
Anasema wakazi wa mji mdogo wa Mirerani walikuwa na hofu ya kutokea wizi majumbani kwao endapo shughuli za madini zingesitishwa kwa ajili ya corona.
Meneja wa mgodi wa Deo Minja wa kampuni ya California, Omary Mandari anasema anaishukuru serikali kwani haikufunga machimbo ya madini hayo kwa hofu ya corona.
Mandari anasema serikali kupitia Rais John Magufuli aliwatoa hofu watanzania na kumtanguliza Mungu kwa ajili ya kupambana na corona hadi ikamalizika.
Anasema utaratibu mzuri wa kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite uliwekwa vizuri kwa usimamizi wa wanajeshi wakiongozwa na kamanda Aidan Ngaraguza.
“Pale kwenye lango la kuingia kukawekwa matenki ya kunawa mikono kwa maji yanayotiririka sabuni na kuvaa barakoa huku vitakasa mikono watu wakitembelea navyo mfukoni,” anasema Mandari.
Anasema hata kwenye migodi yao walifuata utaratibu na muongozo wa serikali wa kuhakikisha wachimbaji wanaachiana nafasi na kuweka ndoo za maji yanayotiririka kwa ajili ya kunawa mikono.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula anawapongeza wachimbaji madini ya Tanzanite kwa namna walivyotekeleza maagizo ya serikali wakati wa janga la Corona.
Chaula anasema alizungumza na wadau wa madini na kuwapa maagizo ya kujikinga wakati ambapo janga hilo lilipokuwa tishio kwao.
“Serikali haikufunga machimbo kwani wachimbaji waliachiwa wafanye kazi ili mradi wanafuata utaratibu wa kujikinga kupitia miongozo ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,” anasema Chaula.
Anasema pia wanashukuru Rais John Magufuli kwa namna alivyosimama kidete kuhakikisha watu hawajifungii ndani kwa saba ya corona.
“Tumeona nchi nyingine watu wanajifungia ndani ili kuogopa corona lakini Rais Magufuli akasimama kidete na kuwaondoa hofu watanzania kwa kujikabidhi mbele ya Mungu ambaye akasikia sala na dua,” anasema Chaula.
Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (Marema) Justin Nyari anasema wanaishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa namna ambavyo walichukulia tatizo la corona kwa kujali watanzania.
Nyari anasema wachimbaji wa madini ya Tanzanite waliendelea na shughuli zao kwa kutekeleza maagizo ya serikali bila machimbo hayo kufungwa.
Ili kuhakikisha sekta ya madini inakuwa salama kwenye kipindi cha magonjwa ya milipuko ikiwemo maambukizi ya virusi vya corona, shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini, likawajengea uwezo wachekechaji 60 wa madini ya Tanzanite kwa kuwapa elimu ya afya na usalama machimboni.
Ofisa miradi wa shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise anasema wachekechaji hao wamepatiwa mafunzo hayo kwa muda wa siku mbili ili kutambua namna ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
Mbise anasema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanachangia kupunguza athari za afya kwenye shughuli za uchekechaji.
Anasema pamoja na kutoa mafunzo hayo pia waliwapatia barakoa 400 kwa ajili ya kujikinga na corona na vumbi wakati wakifanya shughuli zao za uchenjuaji mchanga wa madini ya Tanzanite.
“Pamoja na washiriki hao 60 pia kuna viongozi watano wakiwemo wa serikali hivyo kuwa na washiriki 65 ambao kwa namna moja au nyingine watakuwa mabalozi wazuri kwa wengine,” ansema Mbise.
Mwenyekiti wa wachekechaji wanawake wa Naisinyai, Nairukoki Leiyan anasema mashirika mengine yaige mfano wa Haki Madini katika kuwajali wadau wa madini ya Tanzanite.
Leiyan anasema mafunzo hayo yatawasaidia kufanya shughuli zao ipasavyo na pia barakoa walizopatiwa zitawakinga na vumbi.
Mmoja kati ya wachekechaji hao Isaya Maliaki anasema mafunzo hayo yatawajengea uwezo zaidi wa kufanya kazi zao kwa usalama zaidi tofauti na awali.
Maliaki anasema pamoja na mafunzo hayo pia barakoa waliopatiwa zitawakinga na vumbi wakati wakifanya shughuli zao za uchenjuaji mchanga wa madini ya Tanzanite.
Anasema wachekechaji hao wakitekeleza namna walivyofundishwa watakuwa salama kwani watakuwa wanashika michanga kwa kutumia vikinga mikono wakati wakifanya kazi zao.
Ofisa afya wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Boniface Jacob amewapongeza Haki Madini kwa kuwajengea uwezo wachekechaji hao wa madini ya Tanzanite.
Jacob anasema zaidi ya kuwapa mafunzo ya kuwezeshwa kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona pia barakoa waliopatiwa zitawakinga na vumbi hivyo kuepuka na maradhi ya vifua.