Home Mchanganyiko OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YAOKOA MATRILIONI

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YAOKOA MATRILIONI

0

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju akizungumza leo kwenye mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata akizungumza leo kwenye mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Madai, Deodatus Nyoni akitoa neno la shukrani kwenye mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

Washiriki wa mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

Washiriki wa mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua  mafunzo ya Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

………………………………………………………………………………..

Na Alex Sonna, DODOMA

Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja, Ofisi hiyo imeokoa Sh.Trilioni 11.4 baada ya kushinda kesi ndani na nje ya nchi ambazo zilikuwa zinaikabili serikali huku ikishinda kesi za ndege zilizokuwa zimekamatwa Afrika ya Kusini na Canada.

Wakili Malata ametoa kauli hiyo leo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali na watumishi wengine, yanayofanyika kwa siku tatu Jijini Dodoma.

Amesema Ofisi hiyo inawajibika kila siku kwa mashauri yaliyofunguliwa dhidi ya serikali, na ilianza kazi mwaka 2018 na katika mwaka wa fedha 2019/20 ambao umeisha Juni, kwenye utekelezaji wa majukumu yake imeokoa fedha hizo.

Ameeleza kuwa kuna mali za serikali zilikuwa zimekamatwa nje ya nchi mojawapo ilikuwa ni ndege hizo ambapo ofisi hiyo iliendesha mashauri na mali hizo kuwachiwa baada ya kushinda kesi hizo.

“Ofisi hii pia imerejesha serikalini mashamba  106 ambayo yalikuwa yametwaliwa na watu wenye nia mbaya dhidi ya mali za serikali, vile vile kuna viwanja, hoteli na nyumba mbalimbali ambazo zilikuwa zimetwaliwa na watu wasio na nia njema na serikali nazo zimerejeshwa ikiwemo Hoteli ya Mbeya na ipo mikononi kwasasa mwa Shirika la Reli Tanzania,”amesema.

Amesema kutokana na mafanikio hayo wameona ni vyema kuendelea kuwajengea uwezo Mawakili ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Mafunzo haya yameandaliwa ili kuwaongezea ujuzi katika maeneo mbalimbali baadhi ya maeneo ni ustadi wa ukusanyaji wa maelezo na kuandaa kesi, stadi za kuandaa hati na utetezi, uandishi wa maelezo na ushahidi, kuongeza mashahidi kutoa ushahidi mahakamani, ushahidi wa kielektroniki, wajibu wa mawakili kwa serikali na mahakama,jamii kwa ujumla,”amesema.

Amebainisha pia suala la miiko na maadili ya mawakili hao na matarajio yao ni kwamba baada ya mafunzo hayo Mawakili wa serikali na watumishi wengine kwenye mafunzo hayo watakuwa wamepata stadi stahiki zitakazowaongezea uwezo wa uendeshaji mashauri mahakamani.

Akifungua mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju, amesema serikali inaamini mafunzo hayo yataleta manufaa makubwa kwenye utendaji kazi wao na kuwataka Mawakili kuhoji wakufunzi pale ambapo hawajaelewa ili kuongeza ufanisi kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.