Home Mchanganyiko MAAJABU YA FUKWE ZA MHALO ZIWA NYASA, UNAONA NCHI MBILI KWA WAKATI...

MAAJABU YA FUKWE ZA MHALO ZIWA NYASA, UNAONA NCHI MBILI KWA WAKATI MMOJA

0

……………………………………………………………………….

Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imebarikiwa kuwa na fukwe za asili
katika ziwa Nyasa ambazo hazifanani na fukwe nyingine zozote duniani na
endapo zitaendelezwa zinaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa
serikali na wananchi.
Fukwe ya Mhalo iliyopo katika kijiji cha Ruhekei Kata ya Kilosa
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imeendelezwa kwa kujengwa vivutio vya
utalii pamoja na hoteli ya Mhalo beach Lodge iliyojengwa mwambao mwa
fukwe za Mhalo.
Benado Lisambo ni Meneja wa Mhalo Beach Lodge anasema fukwe hizo
zina maajabu ambayo hayawezi kupatikana sehemu nyingine hali ambayo
inavutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kufanya utalii na kupata
huduma zote zinazostahili kwa watalii.
Anakitaja kivutio kikubwa katika fukwe hizo kuwa ni mtalii anaweza kuona
mipaka miwili ya nchi mbili za Malawi na Msumbiji kwa wakati mmoja
jambo ambalo linawavutia watalii wengi wanaotembelea fukwe hizo.
“Sisi wilaya Nyasa tuna bahati sana,ukiwa hapa Mhalo beach ukiangalia
kusini unaona milima ya nchi ya Msumbiji na ukiangalia Magharibi unaona
milima ya nchi ya Malawi,wakati wa usiku unaweza kuona taa za magari
katika nchi hizo kwa kweli inavutia sana’’,anasisitiza Lisambo.
Hata hivyo anasema fukwe yote ya Mhalo inavutia wageni wengi wa ndani
na nje ya nchi kwa sababu haina uchafu,maji yake ni maangavu hali
ambayo inamwezesha mtalii kuwaona samaki wanavyotembea ndani ya
maji katika ziwa Nyasa.
Kulingana na Meneja huyo,toka fukwe ya Mhalo hadi mpakani na nchi ya
Msumbiji ni umbali wa kilometa 30 na kwamba unaweza kusafiri kwa boti
kupitia ziwa Nyasa na kwamba kusafiri kwa boti toka fukwe ya Mhalo hadi
nchini Malawi ni safari ya saa sita.
Anawataja watalii ambao wametembelea fukwe za Mhalo kuwa wametoka
nchi za Ujerumani, Italia, Uingereza, Marekani, Japan,Afrika ya
Kusini,Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na kwamba wanapokea pia watalii
wengi kutoka ndani ya nchi.
“Watalii wakifika hapa Mhalo beach kuna vivutio vingi, wanaweza kufanya
utalii wa kuogelea,kupanda milima ya Livingstone, kutembea ufukweni

kilometa mbili,kuona ngoma za asili mwambao mwa ziwa Nyasa,ikiwemo
ngoma ya mganda,kioda na lindeku na kufanya safari za majini kwa
kutumia boti’’,anasema Lisambo.
Joseph Ndomondo Mwongoza watalii Mkazi wa Liuli ziwa Nyasa anasema
fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania ni bora zaidi kwa kuwa ni za
asili ambazo zimetengenezwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe.
“Fukwe za ziwa Nyasa upande wa Malawi zimetengenezwa toka kingo za
milima hivyo zimechimbwa hali ambayo inadhihirisha ubora wake hauwezi
kulingana na fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania’’,anasema
Ndomondo.
Afisa Maliasili na Utalii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Bugingo
Bugingo anasema ziwa hilo limebarikiwa kuwa na fukwe nzuri za asili na
zinazofaa kwa uwekezaji kwenye sekta ya utalii hivyo ametoa rai kwa
wawekezaji kuwekeza ziwa Nyasa.