*****************************************
Na Munir Shemweta, WANMM BABATI
Ofisi ya Ardhi mkoa wa Manyara imeanza mkakati maalum wa kwenda ofisi za ardhi katika halmashauri za wilaya kuzifuatilia Hati za Ardhi ambazo haziwasilishwi kwenye ofisi hiyo kwa wakati ili kujua changamoto zake na kuzitafutia ufumbuzi.
Mkakati huo unafuatia Ofisi ya Ardhi mkoa wa Manyara kuzishambulia kwa nguvu Hati zilizopelekwa katika ofisi hiyo zikiwemo zilizokuwa na marekebisho na kuzimaliza zikitokea iliyokuwa ofisi ya ardhi kanda ya Kaskazini (Moshi) iliyojumuisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Hayo yalibainishwa leo tarehe 15 Oktoba 2020 na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Manyara Leonard Msafiri wakati akielezea utendaji kazi wa ofisi yake tangu na kuzinduliwa rasmi julai mwaka 2020 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
“Sasa kama ofisi ya ardhi mkoa wa Manyara tumeamua kuja na mkakati maalum wa kwenda katika wilaya kuzitafuta hati zilizopo kule, kwa nini haziji na why haziendi kwa kasi kubwa”. Alisema Msafiri.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi huyo wa Ardhi mkoa wa Manyara, tayari ofisi yake imeanza kuzifanyia kazi baadhi ya changamoto za sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa huo na kutolea mfano halmashauri ya wilaya ya Babati katika suala la uandaaji ‘deed plan’.
“Katika kutekeleza mkakati wetu sisi tumewapeleka wataalam wetu wawili wa upimaji na ramani kuangalia ramani zinazotakiwa kuandaliwa ramani ndogo ya hati katika halmashauri ya Babati na tutaendelea halmashsuri nyingine.
Alisema, wataalam watakapofika ofisi za ardhi za halmashauri husika wataitisha majalada ya ardhi ya wamiliki walioomba kumilikishwa na kuyafanyia kazi na kuangalia changamoto za msingi kama zipo na yatakapokamilika wataondoka nayo.
Msafiri alisema, ofisi ya ardhi mkoa wa Manyara tangu kuanza kazi Machi mwaka huu imefanikiwa kuandaa na kugawa hati kwa wamiliki wa ardhi takriban 350 na kubainisha kuwa, lengo la ofisi yake ni kuhakikisha hati zote zinazowasilishwa zinakamilishwa ndani ya wiki moja na kupelekwa kwa wahusika.
“Hapa tumejiwekea utaratibu wa Hati zinapofika mezani kutoka halmashauri muda wa kushughulikiwa usizidi siku 2 labda pale inapokuwa na matatizo makubwa na kukamilishwa ndani ya wiki moja ” alisema Msafiri.
Akigeukia suala la urasimishaji katika mkoa wake, Msaifiri alisema zoezi hilo linaendelea vizuri na kueleza kuwa changamoto kubwa iliyojitokeza ni kwenye halmashauri ya Kiteto iliyokuwa ikichukua asilimia 15 ya fedha inayotolewa na wananchi kwa mkandarasi na kufifisha kasi ya zoezi hilo.
Kwa mujibu wa Msafiri, ofisi yake ilitembelea uwandani na kuzungumza na uongozi, mkandarasi na wataalam wa ardhi kuhusiana na suala hilo na kuagiza kusitishwa makato hayo na fedha kidogo zinazotolewa na wananchi iingie kwenye mradi ukamilike na Hati zikitolewa zitaandaliwa ankara zitakazoingizwa madeni na asilimia itoke wakati kazi imekamilika.
Kuhusu migogoro ya ardhi, alisema tangu kuanzishwa ofisi ya ardhi mkoa wa Manyara wamehakiki mashamba yote na kuanza kuyafanyia kazi yenye migogoro na kutolea mfano wa shamba liliko Mawemairo eneo la Magugu lenye ukubwa wa ekari 111 ambalo wananchi walilalamika kuwa wamenyanganywa. Msafiri alisema baada ya kulikagua eneo hilo kwa ushirikiano na walalamikaji walibaini kuwa shamba hilo halikuvamiwa bali uelewa mdogo wa walalamikaji ndiyo uliosababisha mgogoro huo.
Kwa mujibu wa Msafiri, walalamikaji ambao ni wananchi wa maeneo hayo waliishukuru ofisi ya ardhi mkoa wa Manyara hasa Kamishna Msaidizi kwa kuwapa ufahamu kuhusiana na eneo hilo na kueleza kuwa awali ilikuwa ngumu kwao kuongozana na Kamishna wa Ardhi hatua kwa hatua na kuingia vjijini hadi kufikia mahali kujua kitu gani wanachoenda kukifanya.
Katika hatua nyingine, ofisi ya ardhi mkoa wa Manyara imeamua kuwapelekea baadhi ya wamiliki wa ardhi hati zao majumbani.
Wamiliki waliopelekewa Hati zao ni Bw Mustafa Mbaga anayeishi eneo la Mlandege Babati na
Aminiufoo Dominick Uronu mkazi Babati mtaa wa Kwere ambapo wamiliki hao walikabidhiwa hati zao na Msajili Msaidizi wa Hati Ofisi ya Ardhi mkoa wa Manyara Elias Ndalichako.
Msajili Msaidizi wa Hati mkoa wa Manyara Ndalichako alisema, ofisi yake imeamua kuwapelekea hati majumbani baadhi ya wamiliki kama ishara ya kuonesha kuwa sasa huduma za sekta ya ardhi zimesogezwa karibu na wananchi. Kwa mujibu wa Ndalichako, uamuzi huo unatoa fursa ya ofisi yake kutoa elimu sambamba na kupata changamoto zinazowakabili wamiliki katika sekta ya ardhi.
Hata hivyo, wamiliki waliokabidhiwa hati waliishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi ya ardhi mkoa wa Manyara kwa kuwapatia Hati walizozieleza kuwa wamezipata kirahisi ukilinganisha na wakati huduma za sekta ya ardhi zilipokuwa zikipatikana ofisi ya Kanda mkoani Kilimanjaro.
Walisema, ilikuwa usumbufu mkubwa kuhangaikia Hati na huduma nyingine za ardhi mkoani Kilimanjaro ambapo walisema mbali na usumbufu wa umbali lakini pia uliwaongezea gharama nyingine za kusafiri na malazi walipokuwa wakifuatilia hati.