*********************************
NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Hussein Ali Mwinyi, amesema endapo atapata nafasi ya urais, atahakikisha sheria na sera za michezo nchini zinafanyiwa mabadiliko ili ziendane na mahitaji ya michezo.
Alisema hatua za maendeleo katika michezo zitafikiwa kama sheria ya michezo ya mwaka 2010,itakuwa inatekelezeka na inabeba maslahi ya wanamichezo.
Hayo aliyaeleza katika mwendelezo wa ziara zake za kukutana na makundi ya kijamii, ambapo amekutana na viongozi na wadau wa vyama vya michezi kisiwani humo katika hoteli ya Misali Pemba.
Alieleza kuwa katika kuleta mageuzi ya kimaendeleo katika sekta ya michezo nchini ni lazima kuzingatia mambo matatu ambayo ni kutazama upya sera na sheria ya michezo,serikali kuwezesha michezo na kuibua vipaji kuanzia mashuleni.
Alisema lazima makampuni na wafanyabishara wakubwa wachangie kudhamini michezo kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.
Alieleza kuwa bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ambayo ni sehemu ya upatikanaji wa ajira kwa vijana wenye vipaji.
Katika maelezo yake mgombea huyo alisisitiza kuwa lazima michezo iwezeshwe kwa serikali kuweka fungu maalum kwa ajili ya michezo, kushirikisha sekta binafsi kutoa udhamini na kwamba yeye atatafuta wadhamini wa kudhamini sekta hiyo.
Alisema ni lazima kuviwezesha kifedha vilabu vya michezo nchini ili viweze kujiendesha vyenyewe na kusimamia ipasavyo michezo.
Alisema licha ya kuwepo na kanuni zinazoelekeza serikali kutoingilia masuala ya ndani ya michezo lakini kwa utawala wake atahakikisha anaondosha vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa taasisi za michezo hali inayopelekea sekta hiyo kudumaa.
Akizungumzia suala la ligi kuu ya Zanzibar ya mpira wa miguu, alisema ni aibu kubwa ligi hiyo kukosa wadhamini wakati wapo wadau wengi wenye uwezo wa kudhamini ligi hiyo.
Pamoja na hayo alieleza kuwa wakati umefika wa Zanzibar kuwa na vituo maalum ya kufundisha michezo ili watoto wapate mafunzo ya michezo wakiwa wadogo kwa lengo la kukuza vipaji vyao.
“Tushirikiane kwa pamoja katika kuleta maendeleo ndani ya sekta ya michezo kwani michezo ni ajira,michezo ni afya,michezo inajenga mahusoiano mazuri ya kitaifa,kikanda na kimataifa.”, alisema Dk.Hussein.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,alisema CCM imeendelea kuwa karibu na makundi yote ya kijamii.
Alisema suala la michezo halina chama kwani linagusa maisha ya kila mwananchi hivyo wanamichezo hao wanatakiwa kupima sera za CCM kasha wakafanya maamuzi sahihi.
Naye Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar Salum Ubwa alisema mchezo wa mpira miguu ni sehemu ya ajira kwa vijana visiwani Zanzibar na kwamba pia kwenye eneo hilo lina changamoto.
Alisema miongoni mwa changamoto za michezo ambazo zinawakumba wanamichezo hao mgombea huyo ataelezewa na wanamichezo.
“Hii ni fursa adhimu sana kukutana na mgombea wa urais
na kwamba wadau wa michezo wataeleza changamoto mbalimbali za michezo ambazo tuna amini utatutafutia ufumbuzi,”alisema
Kwa upande wake Seif Mohamed Seif akitokea chama cha mpira wa miguu Zanzibar (ZFF) alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar akumbuke kukutana na wana michezo visiwani Zanzibar.
Alisema ZFF ina tatizo kubwa la kiutendaji kutokana na uvunjifu wa katiba na kanuni na kwamba serikali atakayoiongoza inapaswa kuwekeza kwenye sekta ya michezo.
“Niombe jambo moja kwako Dk.Mwinyi katika uongozi wako kila wilaya kuwepo na shule za michezo ‘Sports Academy’ kuna wilaya 11 lakini najua si rahisi kuanza kwa zote lakini tunaweza kuanza na baadhi,”alisema
Alisema katika uongozi wako Wizara itakayoshughulikia Michezo ishirikiane na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha somo la michezo lifundishwe ipasavyo.
“Pia tuwe na michepuo ya michezo ambao mwanafunzi akiingia kidato cha kwanza awe anasomea michezo hadi kidato cha tano na cha sita kuwepo na michepuo ya michezo na pia tuviombe vyuo vikuu vya Zanzibar kuanzisha mafunzo ya michezo na kwamba kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeweza kuwekeza,”alisema
Alisema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar ahakikishe anaongeza bajeti ya Wizara ya Michezo na kwamba ikiwezekana vyama vya michezo pia vipewe ruzuku kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
“Pia hata katika ofisi za Mkuu wa mkoa na wilaya kuwepo kwa fungu maalum ambalo litasaidia kwenye shughuli za michezo kutokana na kuwa kuna kuwepo na mashindano ya Tanzania Bara ambayo yanahusisha timu za ligi za wilaya na mikoa hivyo wakiambiwa waandae timu hawatapata tabu,”alisema
Kwa upande wake Mzee Ali Abdallah ambaye ni mwalimu wa mpira wa miguu alisema changamoto za michezo ya mpira ni kutokuwepo kwa fursa za mafunzo ya michezo ya mpira wa miguu katika ngazi zote kutofanyika kisiwani Pemba.
Alisema alichojifunza ni kuwa hakuna mazingira rafiki sana kwa walimu wa kisiwa cha Pemba na kwamba ana amini kuwa katika uongozi wake fursa za mafunzo za walimu wa michezo ya mpira zitapatikana kisiwani Pemba .
Katika maelezo yake alisema ni wazi kuwa timu za mpira za kisiwani Pemba zimekuwa zina changamoto hasa katika uundaji wa timu ya Taifa na kwamba kumekuwa na mazoea wachezaji wanaocheza timu za Tanzania Bara ndiye mchezaji wa timu wa taifa.
“Mara nyingi kumekuwa na uteuzi wa timu ya taifa huku wakibezwa wachezaji wa timu ya visiwa vya Zanzibar na hasa wachezaji wa timu za kutoka kisiwa cha Pemba wamekuwa na idadi ndogo ya uundaji wa timu ya taifa,”alisema