*********************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi,amesema ana dhamira ya kunyanyua uchumi wa kila mwananchi.
Alisema mipango hiyo inahitaji kuwa na mipango endelevu ya kujenga uchumi kwa kuhakikisha zinajengwa bandari mpya kubwa kwa Unguja na Pemba.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na mabalozi wa mashina ya CCM ya mkoa huo huko katika Ukumbi wa Fidel Castro Chake Chake Pemba.
Dk.Mwinyi,alisema zikijengwa bandari zenye viwango vya kimataifa zitatoa ajira na kuongeza kipato cha nchi.
Alieleza kuwa katika vipaumbele vyake amejielekeza kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya,shule na upatikanaji wa maji safi na salama.
Pamoja na hayo alisema lazima miundombinu ya barabara na nishati ya umeme ziimarishwe ili kurahisisha shughuli za uzalishaji.
Alisema kuwa amejipanga katika kuhakikisha dhana ya uchumi wa bahari (blue economy), inatoa matokeo chanya kwa wananchi.
Alisema Zanzibar ikiwa ni nchi ya kisiwa ni lazima iwanufaishe, wananchi ambao ndio walipa kodi na wadau wa kwanza wa maendeleo nchini.
Alisema endapo atapewa ridhaa ya kuongoza nchi atahakikisha makundi yote yakiwemo ya wafugaji,wakulima,wafanyabiashara,wavuvi na makundi mbalimbali ya wananchi wote watazingatiwa katika ujenzi wa Zanzibar yenye uchumi imara.
katika maelezo yake Dk.Mwinyi,alisema katika ujenzi wa nchi kila mwananchi ana wajibu wa kutoa mchango wake wa katika ukuaji wa uchumi.
Dk.Mwinyi,aliipongeza serikali ya awamu ya saba kwa utekelezaji mzuri wa ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ambayo imetekeleza miradi mingi ya maendeleo.
Aliwaomba mabalozi hao kuendelea kuhamasisha wananchi ili wajitokeze kwa wingi kukipigia kura nyingi chama cha mapinduzi ifikapo octoba 28, 2020.
Sambamba na hayo aliwasihi Wana CCM walinde na kutunza amani ya nchi huku wakijiepusha kuingizwa katika mitego ya wapinzani ya uvunjifu wa amani nchini.
Alisema kwamba serikali ijayo ya awamu ya nane itakuwa karibu zaidi na mabalozi kwani wao ni viongozi muhimu katika ushindi na uhai wa CCM kwa kipindi cha uchaguzi.
“Nimeambiwa changamoto nyingi zinazowakabili wananchi hivyo ahadi yangu kwenu naomba mniamini kwa kunichagua ili niwatumikieni kwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zenu.”,alisema Dk.Mwinyi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,alisema mabalozi wa mashina ya CCM ni jeshi la kisiasa la kupigania ushindi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba Yussuf Ali Juma amempongeza mgombea urais Dk.Hussein kwa maamuzi yake ya kukutana na mbalozi wa mashina ya CCM kwa ajili ya maandalizi ya ushindi wa chama.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Ali Mohamed alisema kuwa chama kimejipanga vizuri kwa kuhakikisha kinashinda majimbo tisa yaliyomo ndani ya mkoa huo.
Wakitoa maoni yao baadhi ya mabalozi hao walisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wanahitaji ulinzi uimarishe.
Walisema kuwa wanahitaji vitambulisho maalum vya kuwatambulisha pindi wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumi yao ya kila siku.
Jumla ya mabalozi 475 wa mkoa huo wameudhuria katika kikao hicho cha kuhamasishana kuelekea uchaguzi mkuu.