Wananchi wa Kijiji cha Mtamaha wakiwa kwenye mkutano wa kupatiwa elimu hiyo ya mpiga kura.
Na Waandishi Wetu, Singida.
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Women Wake-Up (WOWAP) kwa
wiki mbili mfululizo limeendelea kusambaza elimu ya uraia ya Mpiga Kura kwa wananchi
wote wa mkoa wa Singida na vitongoji vyake, lengo likiwa ni kuhakikisha kila
mwana-Singida anatumia haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi sahihi
kuelekea uchaguzi mkuu.
Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka WOWAP, Issah Shayo alisema azma hasa ya mafunzo hayo ni
kuelimisha na kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wao muhimu wa kuhakikisha
wanachagua viongozi bora kwa maendeleo yao katika muktadha wa kauli mbiu isemayo
‘Kura yako, Sauti yako’
“Tunawasihi wananchi wote wa Singida, ifikapo Oktoba 28
twendeni tukapige kura ili kupata viongozi watakaoamua mustakabali wa maisha
yetu na vizazi vyetu…kumbukeni kura yako ndiyo sauti yako,” alisema Shayo.
Alisema shabaha ya mafunzo hayo ni kuhamasisha na kuchochea
kasi ya ongezeko la wananchi wengi zaidi kutambua haki yao ya kuchagua na
kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa kwa uratibu wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi.
Mpaka sasa shirika hilo linaendelea kutoa mafunzo hayo
katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye majimbo ya Singida Mjini, Singida
Vijijini, Singida Kaskazini, Singida Magharibi, Manyoni Mashariki, Iramba
Mashariki na Magharibi.
“Tunapita kwenye mikusanyiko na kufanya mikutano na wananchi
na kuwapatia elimu hii ya uraia, na
tunashukuru kila tunapopita mwamko ni mkubwa. Ujumbe wetu mkubwa kama
shirika la WOWAP ni kuwasihi wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura wasipoteze
fursa hiyo muhimu ifikapo Oktoba 28,” alisema Afisa Utawala wa Shirika hilo,
Loveness John.