Home Mchanganyiko MWALIMU NYERERE NA NDOTO JUU YA RAIS MAGUFULI

MWALIMU NYERERE NA NDOTO JUU YA RAIS MAGUFULI

0

……………………………………………………………………………

Na Lilian Shirima-MAELEZO

Ni miaka 21 sasa tangu Watanzania tumpoteze Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere – Muasisi wa Taifa letu la Tanzania aliyeaga dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mt. Thomas iliyopo London, Uingereza.

Katika Kipindi chote hicho Watanzania tunaendele kumkumbuka kwa maono aliyokuwa nayo juu ya nchi yetu lakini pia uhitaji wa kiongozi mzalendo, mwadilifu na mwenye utayari wa kuleta maendeleo kwa watu wake ili kukidhi matarajio yao.

Miongoni mwa hotuba zake maarufu ni ile aliyoitoa mkoani Mbeya katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi  Duniani Mei 1, 1995 yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine. Hotuba hiyo ilikuwa ni hotuba yake ya mwisho kabla ya kufanyika kwa mara ya kwanza Uchaguzi Mkuu  katika mfumo wa vyama vyingi vya kisiasa nchini.

Pamoja na kwamba Mwalimu alizungumzia masuala ya wafanyakazi, maendeleo na kukemea dosari zilizoanza kujitokeza nchini, kwa hisia pia alisisitiza wajibu wa viongozi watakaochaguliwa kuanzia ngazi ya  Diwani, Mbunge hadi  Rais  katika kutatua matatizo ya jamii zao.

Katika hotuba hiyo alisema, “Tunataka mtu anayetaka kuwa rais wetu ajiulize anataka kuifanyia nini nchi yetu na sio nchi yetu itamfanyia nini?” swali alilomtaka kila anayetaka kuwa mgombea wa chama chochote kujiuluza kwa dhati kabisa.

Aidha, Mwalimu alitanabaisha kuwa mgombea atakayechaguliwa akerwe na hali ya umasikini wa Watanzania na kwamba kero hiyo imsukume kuwa tayari kuishughulikia iwe  ni katika ngazi ya udiwani, ubunge na urais.

Vilevile, alionya wagombea  kuwa Ikulu si mahali pa kukimbilia isipokuwa ni mahali ambapo unakutana na matatizo mengi ya wananchi kama vile njaa, umaskini na huna budi kuyatatua matatizo hayo kwa manufaa ya taifa zima.

“Ukiona mtu anapakimbilia, na hasa anapotumia vipesa kwenda Ikulu mtu huyo ni wa kuogopa kama ukoma!……Mtanzania wa leo hawezi kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa, na kama kanunuliwa atataka kuzilipaje, … kama kakopa atazirudishaje?”, alisema Mwalimu.

Tunapoelekea katika uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu, tunakumbuka namna Mwalimu Nyerere alivyoipenda  nchi yake, alijitoa kwa nadharia na vitendo , alikuwa mshauri katika masuala mbalimbali kuanzia siasa, uchumi, na hata masuala ya kijamii.

Mwalimu aliipenda nchi yake na alikuwa tayari kusaidiana na viongozi wengine wanaoijenga nchi bila kujali itikadi za kisiasa au kidini. Alikuwa kiongozi mkweli asiyetetereka kwani alikuwa tayari kuwapinga na kuwakemea bila woga viongozi wanaoharibu nchi hata kama wanatoka katika chama chake.

Alitamani kuona taifa linaongozwa na kiongozi mwadilifu, jasiri na shujaa, kiongozi mwenye nia ya dhati ya kupambana na maadui ujinga, maradhi na  njaa ili kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa watu.

Kupitia hotuba zake, ni kama vile Baba wa Taifa aliota ndoto juu ya Rais wa Awamu ya Tano, Mh. John Pombe Magufuli.  Miaka mitano iliyopita Watanzania tulipiga kura ya kumchagua rais huyu ili aiongoze  nchi yetu kwa kipindi cha miaka kumi kwa mujibu wa sheria ikiwa na maana miaka 5 awamu ya kwanza na miaka mingine mitano kama atachaguliwa tena kwa ridhaa ya wananchi.

Katika uchaguzi  wa mwaka 2015, uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti, mgombea wa urais wa Chama tawala nchini (Chama Cha Mapinduzi-CCM) alitangazwa kuibuka mshindi wa  kiti cha urais.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),  chini ya Mwenyekiti wa Tume hiyo kwa wakati huo, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva,  ilimtangaza rasmi Mh.  John Pombe Magufuli kuwa  ndiye rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na kwamba ameshinda kwa asilimia 58 za kura zote zilizopigwa dhidi ya mshindani wake  wa karibu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye alipata asilimia 40 ya kura zote zilizopigwa.

Tangu alipoapishwa rasmi, tarehe, 5 Novemba, 2015, Rais Magufuli amedhihirisha  kwa vitendo kuwa ile ndoto ya Baba wa Taifa katika hotuba yake ya Mei Mosi, 1995 sasa imetimia  kwa kuwa amepatikana kiongozi anayeguswa na shida za wanyonge, sifa ambayo Baba wa Taifa alikuwa akisisitizia.

Katika hotuba yake ya kwanza aliyoitoa Jijini Dodoma, tarehe, 22, Novemba, 2015, wakati wa uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano Tanzania Rais John Magufuli aliyataja maeneo yaliyolalamikiwa na wananchi akiwa katika kampeni kuwa ni pamoja na rushwa, ubadhirifu, urasimu, upotevu wa mapato, uzembe sehemu za kazi na migogoro ya wakulima na wafugaji. 

Maeneo mengine ni ukosefu wa huduma muhimu za kijamii kama vile maji, nishati,afya, elimu ,ajira na  ubovu wa miundombinu. 

Aidha, Rais Magufuli aliahidi kushughulikia matatizo ya wananchi bila kujali itikadi za vyama vya siasa isipokuwa kutanguliza nchi mbele kwa kuwa matarajio na matumaini ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ni makubwa.

“Wanachotaka kuona wananchi  ni nchi yetu kupiga hatua kubwa za maendeleo zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na kero zao. Nyie na mimi baada ya miaka mitano tutapimwa kwa namna tukakavyokuwa tumetekeleza mambo ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu”, alisema Rais Magufuli.

Wakati  tunaenzi mawazo na nasaha za Baba wa Taifa baada ya miaka 21 tangu alipofariki, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais  Magufuli  imefanikiwa kuleta maendeleo kwa wananchi kwa kipindi kifupi.

Aidha, imeimarisha nidhamu na uwajibijaki kwa watumishi wa umma, imeondoa urasimu,  na hivyo kupunguza rushwa kwa kiasi kikubwa ndani ya Serikali, imepunguza matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima kama vile kupunguza safari za nje za viongozi, kupunguza sherehe na warsha na kuelekeza fedha zilizokuwa zitumike kwenye huduma za jamii.

Kwa upande wa kilimo, Serikali ya Awamu ya Tano, Imeimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima ikiwa ni pamoja na  kuimarisha vyama vya ushirika ili kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija. 

Kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuanzia mwaka 2015 hadi  mwezi,Aprili, 2020, vijiji 9,112 kati ya 12,268 ambavyo ni sawa na asilimia 80 vimepatiwa umeme .  Aidha sekta ya afya imeimarishwa ambapo upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na huduma za matibabu zimekuwa za uhakika ikiwa ni pamoja na kujenga na kukarabati vituo vya afya, hospitali za Wilaya, hospitali za Rufaa na za Kanda pamoja na kuongeza huduma za kibingwa ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi. 

Hatua nyingine zilizochukuliwa katika kuwaletea maendeleo wananchi wa kada mbalimbali  ni pamoja na kuimarishwa kwa miundombinu, sekta ya usafiri na usafirishaji, uanzishwaji wa masoko ya madini, utoaji wa risiti za kieletroniki, urasimishaji wa biashara zisizo rasmi zenye mtaji chini ya shilingi milioni. 4 kwa kuwatengenezea wajasiriamali wadogo vitambulisho.

Vilevile, katika Awamu hii,  tumeshuhudia  Serikali ikihamia Dodoma , ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa Bonde la Rufiji wenye uwezo wa kuzalisha megewati 2,115 unaoendelea kwa gharama ya shilingi trilioni 6.5 na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) itakayogharimu shilingi.  trilioni 7.  Aidha, viwanda 8,877 vikiwemo  vidogo, vikubwa na vya kati vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali nchini 

Mafanikio haya yanatokana na ujasiri wa Rais Magufuli kufanya maamuzi magumu ambayo yalisuasua tangu uongozi wa Baba wa Taifa lakini sasa yametekelezeka kwa ufanisi 

Ni kutokana na sababu hizi, Julai mwaka huu wa 2020, Benki ya Dunia iliitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yenye uchumi wa kipato cha kati wa  dola 1,006 hadi 3,995 kwa mwaka. Hali hii inayoelezwa kuwa imetokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati iliyoweza kukuza ajira kwa wananchi na kuinua  vipato vyao.

Tunapoadhimisha miaka 21 ya kifo cha Baba wa Taifa, tunayo sababu  ya  kujivunia mafanikio yaliyopatikana sasa nchini kwa kuwa ndoto ya  Baba wa Taifa ya mwaka 1995,  Watanzania tunaiishi kwa vitendo hasa tunapoangalia hatua kubwa za maendeleo ambzao nchi yetu imezipiga kwa muda mfupi.  Ni hali halisi. 

MWISHO