Home Mchanganyiko Jaji ashindwa kusikiliza maombi ya benki ya NBC

Jaji ashindwa kusikiliza maombi ya benki ya NBC

0

Na

***********************************

Ahmed Mahmoud,Arusha

Mahakama kuu ,masijala ndogo ya kazi Arusha, imeshindwa kusikiliza maombi ya pingamizi ya kuzuia kuuzwa kwa Mali za hotel ya Impala yaliyowasilishwa na Benki ya Biashara ya NBC kupitia wakili wake kutokana na mafungufu kadhaa yaliyopo katika shauri hilo.

Maombi hayo madogo namba 63/2020 yaliyoletwa mahakamani hapo kwa hati ya dharura ,mbele ya Jaji Yohane Masara,ambapo wakili anayeiwakilisha benki ya  benki ya NBC ,Willbard Masawe kutoka kampuni ya uwakili ya Mawala aliishawishi mahakama hiyo kupokea maombi hayo ya pingamizi na kuyasikiliza .
Hata hivyo ,jaji Masara alibaini kuwa maombi hayo yalikuja kinyume na utaratibu na kuwa na mapungufu na kumtaka mleta maombi kuyafanyia marekebisho na kuyarejesha upya mahakamani hapo oktoba 20,mwaka huu .
Wakili Masawe alisema kuwa kimsingi mteja wake ambaye ni benki ya NBC anapinga kuuzwa kwa jenereta la hotel ya Impala ambalo hivi karibuni mahakama hiyo iliamuru lipigwe mnada ili kulipa fedha za wafanyakazi zaidi ya 165 wa hotel hiyo wanaomdai mwajiri malimbikizo ya mishahara.
Masawe alibainisha kwamba mteja wake anapinga kuuzwa kwa jenereta hilo kwa sababu hoteli ya Impala.walitumia Mali hiyo kuchukua mkopo kwenye benki hiyo ya NBC na pia mali hiyo ni sehemu ya kesi namba 13/2019 ya madai iliyopo mbele ya jaji Robert Kassim wa mahakama kuu,hivyo uuzwaji wa mali hiyo utaingiliana na shauri ambalo tayari lipo mahakamani.
Awali kaimu afisa kazi mkoa wa Arusha,Emmanuel Mweta aliitaka mahakama hiyo itupe maombi hayo kwa sababu hayana msingi na iamuru taratibu za uuzwaji wa mali za mdaiwa ziendelee kwa sababu wafanyakazi wanahali mbaya kimaisha kutokana na kutolipwa mshahara na mwajiri wao kwa muda mrefu.
Jaji Masara aliahirisha shauri hilo hadi oktoba 20 mwaka huu siku ya jumanne ambapo shauri hilo litatajwa tena .
Hatua hiyo iliwafanya wafanyakazi wa hotel hiyo waliofurika mahakamani hapo kuondoka wakiwa vichwa chini wakinung’unikia jambo hilo.
Mmoja ya wafanyakazi wa hotel ya Impala Jacob Joel  alisema kuwa wameshtushwa na maombi yaliyowasilishwa mahakamani na upande wa benki ya NBC kuzuia kuuzwa kwa mali za mdaiwa na kudai kwamba jambo hilo linazidi kucheleweza hakiyao ya msingi.
Jenereta hilo kubwa aina ya Katapila KV 400 tayari limeondolewa kwa mdaiwa na linashikiliwa na dalali wa mahakama na lilipaswa kupigwa mnada novemba 18 mwaka huu .