Mchekechaji wa madini ya Ruby wa machimbo ya Mundarara Wilayani Longido Mkoani Arusha, Martha Ngada akichakata madini ya Ruby
**********************************
Na Joseph Lyimo, Longido
WACHIMBAJI wa madini ya Ruby kwenye machimbo ya Mundarara, Wilayani Longido Mkoani Arusha, wamepatiwa elimu ya kujikinga na magonjwa ya milipuko yaliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Haki Madini.
Akizungumza jana Ofisa miradi wa shirika la Haki Madini, Emmanuel Mbise amesema lengo la kutoa elimu hiyo ni kuhakikisha wachimbaji hao wanafanya kazi zao kwenye mazingira bora.
Mbise amesema miongoni mwa mafunzo waliyopatiwa ni kuepuka magonjwa ya milipuko kwenye machimbo hasa maambukizi ya kifua kikuu na corona.
Amesema ni vyema wadau hao wa elimu kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya milipuko ili waweze kukabiliana wakati wakifanya shughuli zao za uchimbaji.
“Magonjwa ya milipuko kama ya vifua kikuu, corona, kipindupindu ni tatizo kwenye sehemu za mikusanyiko ndiyo sababu tukatoa elimu hii na kuwapa barakoa ya kujikinga na vumbi na magonjwa mengine,” amesema.
Ofisa jinsia na uchimbaji wa shirika la Haki Madini, Joyce Ndakaru amesema jamii ya eneo hilo hasa wanawake wamenufaika na mafunzo hayo.
“Shirika la Haki Madini kupitia mradi wa afya na usalama unaofanikishwa kwenye vijiji vinne vya eneo hilo unawasaidia wana jamii hasa wanawake,” amesema Ndakaru.
Mmoja kati ya wadau wa madini ya Ruby wa eneo hilo, Martha Ngada amesema kupitia elimu hiyo wamefanikiwa kuongeza uwezo wa kutambua namna ya kujikinga na magonjwa ya milipuko.
“Pamoja na kuwa ugonjwa wa corona haujaripotiwa hivi sasa lakini nchi jirani ya Kenya bado wana changamoto hiyo hivyo tunashukuru kwa elimu tuliyopata,” amesema Ngauda.