**************************************
KUMBUKIZI YA MIAKA 21 YA KIFO CHA MWALIMU NYERERE
(Na Jovina Bujulu-MAELEZO)
Kila ifikapo tarehe 14, mwezi Oktoba, Watanzania wanakumbuka kifo cha muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo mwaka huu atatimiza miaka 21 tangu afariki.
Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka 24, Taifa la Tanzania limeshuhudia mafanikio lukuki katika nyanja za kilimo, viwanda, madini, afya, elimu, maji na miundombinu. Mafanikio hayo bado tunayaona yakiendelezwa na Rais wa Awamu ya Tano, Mhe. John Pombe Magufuli.
Mwalimu Nyerere ni miongoni mwa viongozi ambao waliweza kukidhi matarajio ya Watanzania kwa kuzingatia maadili ya uongozi na kujenga umoja wa kitaifa katika watu wa makabila zaidi ya 120 wenye dini tofauti,hivyo kudumisha amani ya katika Taifa la Tanzania hali ambayo imesababisha Tanzania kuitwa “ Kisiwa cha Amani”.
Ni kiongozi aliyebeba historia ya Taifa la Tanzania kwa mawanda mapana kwa sababu huwezi kuitaja Tanzania bila kumtaja Mwalimu Nyerere. Wakati wa utawala wake alichukia rushwa na akapitisha sheria kwamba mtu akila rushwa, aliyetoa na aliyepokea wote watapata msukosuko.
Katika kuzingatia maadili ya uongozi, Mwalimu Nyerere alichukia sana rushwa na aliipiga vita kwa nguvu zake zote. Hali hii ilijionesha awali wakati wa chama kilicholeta uhuru Tanganyika mwaka 1961 wakati huo kikiitwa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambapo katika mojawapo ya ahadi za chama cha TANU ilikuwa inasema, ‘Rushwa ni adui wa Haki, Sitatoa wala Sitapokea rushwa’.
Rushwa ni adui wa haki, na ni kitendo kibaya kwa hiyo watu wanaofanya kitendo hicho ni wabaya sana na kitendo hicho hakifungamani na adili za jamii ya Watanzania kwani kinamfanya mwenye haki kunyang’anywa haki yake.
Kwa kuweka ahadi hii kuwa mojawapo ya ahadi za TANU inaonesha jinsi Mwalimu Nyerere alivyokuwa amedhamiria kuondoa suala la rushwa miongoni mwa jamii ya Watanzania kwani alijua kuwa suala la rushwa ni kinyume cha haki za binadamu na huvunja demokrasia.
Kuchukia kwake rushwa kunaonekana katika hotuba aliyoitoa kwa Waandishi wa Habari mwaka 1995 waliamua kuweka sheria ya kuwafunga jela muda usiopungua miaka miwili watoa rushwa na wapokea rushwa ikiwa ni pamoja na kuwapiga viboko 12 wakati wanaingia jela na vingine 12 wakati wanatoka jela.
“Kwa hivyo, tukatengeneza sheria ili tuwafundishe watu hawa kwamba jambo hili hatulipendi. Ikisha kudhibitika mahakamani kwamba kala rushwa hatukumwachia hakimu uamuzi wa adhabu. Tukasema atakwenda ndani muda usiopungua miaka miwili, atapata viboko ishirini na vinne, kumi na mbili siku anayoingia, kumi na mbili siku anayotoka” alisema Mwalimu Nyerere.
Katika kusisitiza ubaya wa rushwa Mwalimu alisema alitaka watu wajue kwamba watakuwa wakali sana kwa wala rushwa na watoa rushwa ndani ya Serikali maana Serikali ikishakuwa na wala rushwa watu maskini hawatakuwa na kitu bali Serikali itaabudu wenye mali.
Aidha aliwahi kusema kuwa Serikali isiyokusanya kodi ni Serikali corrupt kwa sababu haitaweza kuwabana wafanyabiashara wakubwa ili walipe kodi badala yake itabaki kukimbizana na wafanyabiashara wadogo na kuwabana kulipa kodi huku wafanyabiashara wakubwa wakiachiwa huru kwa kuwa wana uwezo wa kutoa rushwa.
Katika kusisitiza hilo Mwalimu alisema “ Serikali corrupt unadhani imwambieje mwenye mali, imwambie nini? utalipa? Usipolipa utakiona! Atacheka tu huyu. Unaniambia mimi hivyo wewe!. Kesho siji basi. Serikali corrupt haikusanyi kodi, itabaki kufukuzana fukuzana na vijitu vidogo vidogo mabarabarani, basi. Mkishakuwa corrupt mtaabudu wenye mali”.
Maneno hayo yanaonesha nia ya dhati ambayo Mwalimu Nyerere alidhamiria katika kukomesha kabisa suala la rushwa na maneno hayo yanathibitisha ubora wake ikiwa ni pamoja na kujibainisha kuwa kitendo cha kupambana na rushwa kinafungamana na adili za jamii ya Watanzania na ndiyo maana kilianzisha chombo cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alisisitiza ubaya wa rushwa kwa kusema “ Nadhani rushwa lazima ishughulikiwe kwa ukali kwa sababu naamini rushwa na hongo ni adui kwa maslahi ya watu kwa amani kuliko vita na naamini inapaswa ishughulikiwe sawa sawa kama aliyefanya uhaini”
Mwalimu pia, aliwajengea nidhamu ya hali ya juu viongozi wenzake katika utawala wake ambapo nidhamu hiyo iliwafanya wawe wazalendo wa kweli. Alikuwa na sifa ya kuwa muwazi asiyeficha kitu na hakuficha kumpasulia mtu ukweli hadharani. Sifa yake hii ilijenga misingi kwa viongozi waliofanya kazi naye.
Aidha alikuwa ni kiongozi aliyekuwa na kipaji cha uongozi hali iliyofanya kuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi ambaye aliyaishi yale yote ambayo aliyasema na kuyasimamia.
Kutokana na kuchukia rushwa, Mwalimu hakuwa rafiki na watu wenye uchu wa mali na madaraka na alisisitiza kujiepusha na rushwa wakati wa uchaguzi ili wananchi waweze kumchagua kiongozi bora mwenye sifa zinazostahili ambaye atawaletea maendeleo badala ya kuchagua kiongozi kwa sababu amewapa rushwa
Hata baada ya kung’atuka katika uongozi , Mwalimu aliendelea kupiga vita rushwa ambapo katika hotuba yake wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mnamo 1995 wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Nyerere alisisitiza “ Chagueni mpinga rushwa, Watanzania wamechoka na rushwa, huyu atatusaidia kupiga vita rushwa, jibu litoke ndani ya roho yake kwamba ndiyo anaweza”.
Katika kumuenzi Mwalimu Nyerere, tunashuhudia jinsi Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais Magufuli inavyopambana na yale yote aliyoyasimamia Baba wa Taifa, ikiwemo utawala bora, vita dhidi ya rushwa ambapo Taifa linashuhudia kazi kubwa inayofanywa na TAKUKURU kwa kurejesha mali za rushwa na magendo Serikalini, vita ya uchumi ambapo Serikali inasimamia ulinzi wa rasilimali za asili kama vile misitu, madini na wanyama.
MWISHO