NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani ,Muharami Mkenge, amesema ,akichaguliwa nafasi hiyo atakaa na viongozi wa Halmashauri kuelekeza nguvu katika ujenzi wa barabara ya Kiromo mpaka Buma.
Sanjali na hilo pia atasimamia ujenzi wa uzio wa tofari katika mabweni ya sekondari ya wasichana ya Kata ya Kiromo, kwa lengo la kuwakomboa wanafunzi wa kike wanaokabiliwa na vishawishi mbalimbali vinavyokatisha ndoto zao za kielimu.
Mkenge aliyasema hayo kijiji cha Buma, akizungumza na wananchi ambapo alisema , pamoja na eneo la Buma kuwa maarufu kwa uchimbaji wa madini ya mchanga, lakini wananchi wake hawanufaiki na uwepo wa madini hayo, kwani miundombinu ya barabara sio rafiki.
“Hali ya barabara nimeiona kiukweli sio rafiki, niwaombe Oktoba 28 tujitokeze kwa wingi tukampigie kura za kutosha mgombea wa Urais Dkt. John Magufuli, mimi Mbunge pamoja na Salumu Mikugo nafasi ya Udiwani, ili mimi na Mikugo tukasimamie maendeleo ya Kata yetu,” alisema Mkenge.
Pia amezungumzia ujenzi wa barabara ya kutokea Buma kuelekea Sunguvuni itayopewa kipaumbele, kutokana na mikakati ya Serikali ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Makofia, Mlandizi mpaka Mzenge, ambapo pia itaangaliwa ya Sunguvuni kuelekea mtambo wa maji wa Ruvu chini.
“Upande wa Mtambo wa Maji wa Ruvu chini sote tunatambua umuhimu wake, kule ndiko kwenye chanzo cha maji yanayosambazwa maeneo ya Pwani na Jijini Dar es Salaam, kutokana na umuhimu huo kuna haja ya uboreshwa kwa barabara hiyo ili kuwezesha magari kuelekea huko kipindi cha mwaka mzima,” alisema Mkenge.
Kuhusiana na changamoto ya kukosekana kwa uzio shule ya sekondari ya Kiromo, Mkenge alisema kwamba atashirikiana na halmashauri, wananchi pamoja na wadau ili kuhakikisha unajengwa uzio kwa ajili ya kuwakinga wanafunzi wa like na vishawishi vinavyowakabili.
Nae Zaynab Vullu mgombea Ubunge wa Viti Maalumu mkoani Pwani, amewataka wana-Buma kutofanya makosa Oktoba 28 huku akieleza kwamba wagombea wanaotokea vyama nje ya CCM hawana ofisi, pia huonekana kipindi cha chaguzi tu.
Kwa upande wake Salumu Mikugo mgombea Udiwani alisema kuwa wakichaguliwa pia wataelekeza nguvu katika ujenzi wa nyumba ya Daktari katika zahanati zilizopo ndani ya Vijiji vinavyonda Kata hiyo, ili kuwaondolea adha wagonjwa wanaokosa huduma kutokana na wataalamu wa afya kuishi nje ya vituo vyao cha kazi.