*********************************
Mnamo mwezi Desemba 2019, Benki Kuu ya Tanzania ilitoa Taarifa kwa Umma kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 iliyoanza kutumika rasmi tarehe 1 Novemba 2019.
Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ilirejea Kifungu cha
57 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ambacho kinawataka watoa huduma ndogo za fedha wote kuwasilisha maombi ya leseni au usajili Benki Kuu ya Tanzania au kwenye Mamlaka Kasimishwa katika kipindi cha miezi 12 baada ya Sheria kuanza
kutumika, yaani tarehe 31 Oktoba 2020.
Benki Kuu imepokea maombi ya wadau wengi ya kuongeza muda wa usajili na utoaji leseni ili waweze kuwasilisha maombi yanayoendana na matakwa ya Sheria na Kanuni husika.
Hivyo, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda
kuutaarifu umma kuwa tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ya usajili au ya leseni imesogezwa hadi tarehe 30 Aprili 2021.
Matarajio ni kwamba muda ulioongezwa utawawezesha watoa huduma ndogo za fedha katika madaraja yote kufanya maandalizi ya kutosha na kuwasilisha maombi yaliyokamilika na
yanayokidhi matakwa ya Sheria na Kanuni.
Kama ilivyoelekezwa awali, maombi ya usajili au leseni yawasilishwe kama ifuatavyo katika muda wa nyongeza uliotolewa:
1. Watoa huduma ndogo za fedha walio katika Daraja la 2 wawasilishe maombi
yao ya leseni Benki Kuu ya Tanzania Makao Makuu au katika matawi ya Benki
Kuu ya Tanzania yaliyoko Arusha, Mwanza, Zanzibar, Mbeya, Mtwara na
Dodoma.
2. Watoa huduma ndogo za fedha walio katika Daraja la 3 wawasilishe maombi
yao ya leseni katika Ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa, kupitia
mfumo wa kuomba leseni wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika.
3. Watoa huduma ndogo za fedha walio katika Daraja la 4 wawasilishe maombi
ya kuandikishwa katika Ofisi za Serikali ya Mitaa zilizo karibu.
Aidha, Benki Kuu inapenda kuutahadharisha umma kuhusu matangazo na maelekezo yenye kupotosha na kuleta taharuki yanayotolewa na watu wasiokuwa na nia njema.
Benki Kuu inautaka Umma kupuuza matangazo na maelekezo yoyote kuhusu utoaji leseni au usajili wa watoa huduma ndogo za fedha ambayo hayajatoka Mamlaka husika.
Aidha, wananchi wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka husika
pale wanapokutana na changamoto mbalimbali katika mchakato wa maombi ya leseni au usajili wa huduma ndogo za fedha.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
1. Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania, S.L.P.
2939, Dar es Salaam au wasilisha barua pepe kwa [email protected];
[email protected]; [email protected]; na [email protected]
2. Mkurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa, S.L.P 1923, 41185 Dodoma au wasilisha barua pepe kwa
[email protected] au [email protected]
3. Mrajisi, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, S.L.P 201 Dodoma au wasilisha barua
pepe kwa [email protected] au [email protected]