………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Babati
Waelikishaji Jamii wa Mkoa wa Manyara, wamejengewa uwezo wa kutoa elimu ya uchaguzi hasa kwa makundi maalum ya vijana, wanawake na walemavu ambao wana mwitikio mdogo wa kushiriki uchaguzi mkuu kuanzia kwenye kampeni hadi kupiga kura.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Civil Social Protection Foundation (CSP) Nemence Iriya akizungumza mjini Babati, amesema waelimishaji jamii hao hawapaswi kupiga kampeni ya chama chochote cha kisiasa zaidi ya kutoa elimu kwa mpiga kura.
Iriya amesema waelimishaji jamii hao watatoa elimu hiyo kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili walengwa wa makundi hayo na wananchi kwa ujumla wafikiwe na kushiriki uchaguzi huo.
Amesema waelimishaji jamii hao watatoa elimu hiyo kwenye maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ikiwemo katika mikutano ya kisheria ya vijiji, mitaa, vitongoji, sokoni, magulio, minada, nyumba za ibada na kwingineko.
“Pia watatoa elimu hiyo kupitia redio mbalimbali za kijamii ila wasifanye hivyo kwa kupanda kwenye majukwaa ya wagombea wa vyama vya kisiasa wanaofanya kampeni katika maeneo yao,” amesema Iriya.
Katibu wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (Shivyawata) mkoani Manyara, Peter Sanka amesema kupitia mafunzo hayo amejengewa uelewa mkubwa hivyo atatoa elimu ya kupiga kura kwa makundi mbalimbali hususani walemavu.
Sanka amesema walemavu wana haki ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa hivyo kupitia mafunzo hayo atatoa elimu aliyoipata ili waweze kushiriki kwa wingi tofauti na uchaguzi uliopita.
Mratibu wa uchaguzi wa Mkoa wa Manyara, Kennedy Kaganda amesema CSP imepewa kibali na Tume ya Taifa ya uchaguzi kwa ajili ya kutoa elimu ya uchaguzi kwa wananchi wa eneo hilo.
Kaganda amesema kupitia CSP anatarajia wananchi wengi watapata elimu ya uchaguzi ili waweze kushiriki kwenye mikutano ya kampeni na siku ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi.
Muelimishaji jamii kutoka wilayani Simanjiro, Obeid Sarakikya amesema wataitumia kikamilifu elimu waliyoipata kutoka CSP ili jamii ya eneo hilo iweze kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Sarakikya amesema makundi maalum ya wanawake, vijana na walemavu, wataweza kushiriki uchaguzi mkuu endapo watapatiwa elimu ya umuhimu wa kupiga kura.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka wilaya ya Babati, Agnes Chagama amesema watajikita kutoa elimu hiyo kwenye makundi hayo maalum ili washiriki kikamilifu kwenye uchaguzi huu.