NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MKURUGENZI Mkuu wa wakurugenzi wa Njuweni institute na Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Kibaha Independent School (KIPS) Alhaj Yusufu Mfinanga amesikitishwa, na vitendo vya vurugu na uharibifu mkubwa wa mali,,uliofanywa na
wanafunzi nane waliohitimu elimu ya msingi shuleni hapo.
Wanafunzi hao walifanya uharibifu huo
mara baada ya kumaliza mitihani yao ya mwisho,wakati wakiwasubiri wazazi wao ili warudi nyumbani.
Mfinanga alieleza masikitiko yake mjini Kibaha ,wakati wa mahafali ya 15 ya darasa la saba ya shule hiyo.
Alisema ,wanafunzi hao waliharibu baadhi ya vitu ikiwa ni pamoja na kupasua vioo, feni na baadhi ya vifaa vya umeme na mali nyingine na endapo hatua zisingechukuliwa haraka wangeweza kuleta madhara makubwa zaidi.
“Tunawaomba wazazi wa wanafunzi hao watoa ushirikiano kwa uongozi wa shule ili kulimaliza suala hilo na endapo watashindwa kutoa ushirikiano hatua za kisheria zitachukuliwa,”alisisitiza Mfinanga.
Nae meneja wa shule ya KIPS ,Nuru Mfinanga aliwaasa ,wanafunzi wanaobaki wasijiingize kwenye vurugu kama hizo kwani vitendo hivyo ni vibaya na havipaswi kuungwa mkono .
Nuru alisema,ifike wakati wanafunzi wawe na nidhamu kwani bila ya nidhamu hawataweza kupata mafanikio ambapo amewataka wanafunzi hao kuendeleza maadili mema wanayopatiwa shuleni na kuwaasa wazazi kuwasimamia watoto wao.
“Wazazi simamieni watoto wenu ,shirikianeni na walimu,ila pia tushirikiane kulipa ada kwa wakati ili kuondoa usumbufu kwa watoto wetu,alisema Nuru.
Mgeni rasmi kwenye mahafali hayo ,Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Robert Shillingi alibainisha, elimu waliyoipata wanafunzi wanaohitimu msingi ni msingi na mwanga wa maisha yao kwani ulimwengu wa sasa unahitaji wahitimu wasomi wenye elimu na upeo wenye kiwango cha juu.
Shilingi alifafanua, endapo wahitimu wa ngazi mbalimbali watakuwa na elimu kubwa wataweza kutumia changamoto kuwa fursa ili kujikwamua na hali ngumu na kujikuta wakijiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Kwa upande wake mwakilishi wa idara ya elimu msingi ya Halmashauri ya Mjini Kibaha ,Ramadhan Laoga alisema, uwekezaji wa elimu kwa watoto ni urithi ambao hauwezi kupotea.
Laoga”;anasema serikali yoyote makini chaguo la kwanza ni elimu hivyo wazazi wanaowekeza kwa wanafunzi wanakuwa wanaiunga mkono serikali makini inayo simamia elimu kama kipaumbele kwa wananchi wake .