…………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Katibu Mkuu Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewaasaa baadhi ya wadhibiti ubora wa shule nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kuacha lugha za vitisho kwa wateja.
Dkt. Akwilapo aliyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo maalum kwa wathibiti wakuu ubora wa Shule kanda na Wilaya zote Tanzania bara, wapatao 217, yanayofanyika wilayani Bagamoyo kwa muda wa siku tatu .
Anasema,lengo la mafunzo ni kuwaongezea ujuzi wa masuala mbalimbali ya utendaji katika utumishi wa umma na kuwasaidia wathibiti wakuu ubora wa shule kuondoa ama kurekebisha changamoto za kiutendaji ambazo zimekuwa zikiripotiwa kwa uongozi wa wizara mara kwa mara katika maeneo wanayosimamia.
“Wizara imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wadau na watoaji wa elimu kuhusu mwenendo usiofaa wa baadhi ya Wathibiti Ubora wa Shule kutoa lugha za vitisho kwa wateja na wakati mwingine kuwaomba Rushwa ili kufanikisha usajili wa Shule au Vyuo vyao .
“Hii ni kukiuka maadili ya utendaji katika utumishi wa umma kwa kutozingatia sheria, kanuni na maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma na wadhibiti ubora wa elimu wanaofanya vitendo hivi waache mara moja kwani taarifa zako zitakapotufikia hatutasita kukuchukulia hatua za kinidhamu” Amesema Dkt. Akwilapo.
Nae Mshiriki wa Mafunzo hayo Bi. Tatu Tamizi Kutoka Wilaya ya Gairo akizungumza kwa niaba ya Washiriki wenzake wa mafunzo hayo amesema, wanashukuru Wizara ya elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwaandalia mafunzo hayo ambayo wanaamini yatawaongezea weledi na ufanisi katika utendaji kazi wao na hivyo kuboresha utoaji huduma za elimu Nchini.