Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Prosper Buchafwe akitoka kuangalia miundombinu ya mradi wa maji wa Matela wilayani Magu wakati wakikagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza
Wananchi makipata huduma ya kuchota majisafi na salama baada ya mradi wa maji Magu kukamilika na kuanza kutoa maji.
Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maji ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Bw. Prosper Buchafwe (katikati) upande wa kushoto pamoja na viongozi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na RUWASA wakiwa ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Magu Bw. Salum Kally wakijadili masuala yanayohusu sekta ya maji katika Wilaya ya Magu.
……………………………………………………………………………
Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) mkoani Mwanza katika kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi umetekeleza jumla ya miradi ya maji 68 katika mwaka 2019/2020.
Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Mwanza Mhandisi Immaculata Raphael amesema hayo ofisini kwake na kufafanua kuwa kiasi cha shilingi bilioni 15.3 kilipokelewa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maji vijijini, ikiwa ni pamoja na kupanga, kusanifu na kusimamia ujenzi wa miradi mipya, ukarabati wa miundombinu na upanuzi wa miradi ili kuongeza huduma kwa wananchi.
“Miradi iliyotekelezwa imegawanyika katika programu tatu ambazo ni PbR miradi 22, PforR miradi 22 na WSDP II miradi 24 ambapo miradi 21 kati ya 22 katika Programu yaPbR, na miradi 10 kati 24 inayotekelezwa na fedha za Mfuko wa Maji imekamilika na utekelezaji wa miradi 40 upo katika hatua mbalimbali” Mhandisi Raphael amesema.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 mkoa wa Mwanza kupitia (RUWASA) umetengewa shilingi bilioni 15.9 na imepangwa kutekeleza jumla ya miradi 25 ambayo itaimarisha zaidi upatikanaji wa huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 49 hadi kufikia asilimia 65.
Wakati huohuo, mradi wa maji wa Magu upo katika kipindi cha matazamio hadi mwezi Novemba 2020 baada ya kukamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 16.9. na umesanifiwa kuhudumia zaidi ya wakazi laki moja wa mji wa Magu pamoja na vijiji vya Busulwa, Bugabu, Ilungu, Kipeja na Kahangala hadi kufikia mwaka 2040.
Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Gogadi Mgwatu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), amesema mradi wa maji wa Magu ulianza kujengwa tarehe 22 Mei, 2017.