Rais wa Jamhuri ya Malawi akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) alipofika kutembelea bandari hiyo Jijini Dar es Salaam ikiwa ni Moja ya Maeneo aliyoyatembela katika Ziara yake nchini.
Rais wa Malawi Dkt. Lazarus Chakwera na Mkewe Monica Chakwera wakipokea zawadi yenye picha ya Bandari ya Dar es salaam baada ya kutembelea Bandari ya Dar es salaam na kujionea Kituo cha Mizigo cha Malawi.
************************************
Na.Paschal Dotto-MAELEZO
Rais wa Malawi Dkt.Lazarus Chakwera, ametembelea ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) katika eneo la Shaurimoyo na Bandari ya Dar es Salaam kujionea maendeleo ya miradi hiyo ambayo inatekelezwa na Serikali ambapo ujenzi wa gati la mizigo katika bandari ya Dar es Salaam umekamilika katika eneo lenye uwezo wa kubeba magari 600,000 kwa mwaka.
Akizungumza katika ziara hiyo, Rais Chakwera amesema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa maendeleo ya nchi mbili ambapo Watanzania na Wamalawi wanafanya biashara kupitia bandari hiyo.
“Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kwa wananchi wa Malawi kwani inatumika katika maisha yao ya kila siku ya kibiashara kwa kusafirisha mizigo mingi kutoka Tanzania ikiwemo usafirishaji wa mafuta”, amesema Rais Dkt.Chakwera.
Aidha, ametoa shukrani kwa Tanzania kwani nchi hizo mbili zinashirikiana vyema katika masuala ya usafirishaji na kuongeza kuwa Tanzania imetoa upendeleo kwa nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Malawi kwa kutoa eneo la kihifadhia mizigo kutoka Malawi lililoko katika Bandari ya Dar es Salaam (Malawi Cargo Centre).
Ameeleza kuwa Malawi inaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania kuimarisha Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa Bandari ya Mtwara kwani ni muhimu kwa maendeleo ya Malawi hasa kwenye sekta ya usafirishaji.
“Malawi inaunga mkono juhudi za ujenzi na kuimarisha Bandari na huduma za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) hasa kuwepo kwa mchakato wa ufunguzi wa ofisi za TPA mjini Lilongwe, Malawi, hii itawezesha kufanya biashara katika mazingira mazuri baina ya wananchi wa Tanzania na Malawi”, amesema Rais Dkt.Chakwera.
Rais Dkt. Chakwera amefurahishwa na kupata kumbukumbu ya Tanzania kuimarisha mshikamano katika ukombozi wa Afrika hasa nchi za Kusini, kwani Malawi imepata eneo la kuweka mizigo ndani ya Ardhi ya Tanzania lililoko katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema kuwa eneo la bandari limepanuliwa na sasa bandari hiyo ina uwezo mkubwa mara tatu kwa kuegesha magari yanayoshushwa katika meli mbalimbali zinazotia nanga bandarini hapo.
“Bandari yetu imepanuliwa na sasa eneo la kuhifadhia magari unaloliona Mhe. Rais limeongezwa uwezo wake mara tatu, sasa tunaweza kupokea magari 600,000 kwa mwaka, kwa hiyo tutaendelea kuhudumia vyema wateja wetu kama TPA”, amesema Kakoko.
Kakoko ameongeza kuwa, ujenzi wa magati unaoendelea katika bandari ya Dar es Salaam huku magati mengine yakikamilika utaiwezesha bandari hiyo kupokea mizigo mingi kutoka tani milioni 16 za awali hadi tani milioni 24 mwaka 2024, huku bandari hiyo ikitarajia kupokea meli zenye ukubwa wa mita 300 badala ya mita 240 za sasa.
Akifafanua uwezo wa bandari hiyo , Mhandisi Kakoko amesema kuwa uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa ni kupokea meli yenye tani 8,000 badala ya 4,000 za awali na kuongeza kuwa Tanzania itaendelea kuhudumia nchi jirani ikiwemo Malawi kwa kutumia bandari ya Dar es Salaam na Mtwara ili kuimarisha uchumi wa nchi hizo mbili