**********************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema iwapo atachaguliwa atahakikisha anazifanyia kazi changamoto zinazowakabili wawekezaji wa sekta mbali mbali ikiwemo ya utalii ili kukuza sekta hiyoya utalii ambayo inaingiza pato kubwa serikalini.
Ahadi hiyo aliitoa wakati akizungumza na wawekezaji mbalimbali walioekeza Zanzibar katika mkutano uliofanyika katika hoteli ya Park Hayyat Forodhani.
Alisema moja ya changamoto hiyo ni kuimarisha ulinzi na usalama kwa wageni wanaokuja kwa ajili ya utalii pamoja na mali zao kwa kuweka askari maalumu ambao watashughulikia sekta hiyo ya utalii.
Aidha alisema hatua hiyo itasaidia kuwapa hamasa watalii kuingia nchini kwa wingi kutokana na kuimarika kwa ulinzi na salama kwa lengo la kuona pato la taifa linaendelea kukua kupitia sekta hiyo.
“Serikali inawathamini sana nyinyi wawekezaji kwani mnatusaidia kukua kwa pato la taifa hivyo naahidi kwenu kwamba nitakapoingia madarakani tutakuwekeeni mazingira bora ili kufanya kazi zenu bila ya kikwazo chochote,” alisema.
Kwa upande wa suala la rushwa Dk. Mwinyi alisema awamu ya nane itahakikisha inaondoa urasimu wa upatikanaji wa maombi ya vibali vya kuishi kwa wawekezaji hao ili kuweka mpango mzuri wa upatikanaji wa huduma hizo.
Sambamba na hayo Dk. Mwinyi aliwasisitiza wawekezaji kuhakikisha waajiri wazawa katika maeneo yao ili kuona wananufaika na uwekezaji huo.
“Lengo langu pia ni kuona vijana wanapata ajira kupitia sekta hii hasa wazawa kwani kuna changamoto kubwa katika vijiji ninavyopita kulalamikia hili,” alibainisha.
Dk. Mwinyi aliwaomba wawekezaji hao kuendelea kuiamini serikali na kuimarisha amani iliyopo nchini kwani kutokana na kuwepo kwa amani ndio iliyowapa nguvu ya kuwekeza nchini.
“Amani yetu ndio kila kitu kwani bila ya Tanzania kuwa na amani nyinyi wawezekaji hamtokuwa na fursa ya kuwekeza na sisi serikali hatutaweza kufanya maendeleo tunayotarajia kwa wananchi wetu,” alisisitiza.
Nao, wawekezaji hao wameahidi kutoa mchango wao katika kuendeleza maendeleo ya Zanzibar, waliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuthamini mchango wao wa kuwekeza miradi mbalimbali nchini.
Hivi karibuni Dk. Mwinyi alikutana na wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima kupitia jumuiya yao katika hoteli hiyo hiyo na kuwaahidi kuweka mazingira bora ya biashara ili kukuza uchumi wa nchi na wanachama wake.
Aidha mgombea huyo aliahidi kushirikiana na jumuiya za wafanyabiashara ili kutambua changamoto wanazokabilana nazo na kutafuta namba bora ya kuzitatua ili kuwanufaisha wadau wote wakiwemo wakulima watakaoongeza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya chakula na biashara.
Mikutano ya Dk. Mwinyi na makundi mbali mbali ya jamii, siasa na uchumi ni sehemu ya kampeni kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu ambapo mbali ya kuomba kura, hutumia fursa hiyo kusiliza na kupokea changamoto zinazowakabili.