Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Wakurugenzi mbalimbali na wadau wa Mawasiliano wakifuatilia kongamano la Nne la Mwaka la Tehama nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Dkt.Zainabu Chaula akifungua Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe akiwana Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Dkt.Zainabu Chaula wakipata picha ya pamoja na watumishi wa Wizara hiyo pamoja na Wakurugenzi wa sekta za Mawasiliano nchini katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Dkt.Zainabu Chaula akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA EMMANUEL MBATILO)
************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Miundombinu iliyojengwa nchi nzima imewezesha huduma za mawasiliano kuwafikia wananchi wengi katika maeneo mbalimbali ya nchi. Juhudi hizi zimeongeza idadi ya wananchi wanaotumia intaneti kutoka milioni 3.56 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 23 mwaka 2017, idadi ya wenye laini za simu kutoka milioni 2.96 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 48 mwezi Machi mwaka huu 2020.
Ameyasema hayo leo Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe katika ufunguzi wa Kongamano la Nne la Mwaka la Tehama nchini katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Kongamano hilo Mhandishi Kamwelwe amesema Serikali inahakikisha kuweka miundombinu bora, mazingira mazuri ya kiudhibiti katika utoaji wa huduma za mawasiliano kwa ushindani na mfumo madhubuti wa kisheria unaohakikisha kuwa huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Juhudi zaidi za pamoja zinahitajika kuhakikisha kuwa huduma bora zaidi za mwasiliano zenye intaneti yenye kasi zinawafikia wananchi kwa gharama ambazo wengi wanazimudu ili nao washiriki vizuri katika uchumi unaoendeshwa na TEHAMA (digital economy) bila kikwazo”. Amesema Mhandisi Mhandisi Kamwelwe.
Aidha Mhandisi Kamwelwe amesema sekta ya Mawasiliano inaongozwa na Sera ya Taifa ya TEHAMA iliyodhamiria kuifanya Serikali kuwa mfano katika kutumia TEHAMA (a model user).
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Dkt.Zainabu Chaula amesema washiriki wa kongamano hilo watabadilishana uzoefu na kuweza kuendana na kasi ya mabadiliko ya tehama katika kuchochea maendeleo ya jamii na kiuchumi.
Hata hivyo amesema mpaka sasa asilimia 94 ya mawasiliano yametapakaa nchini na maeneo machache ambayo bado hayajashughulikiwa hasa kutokana na jeografia ya nchi yetu lakini katika kipindi hiki tutahakikisha kufikia asilimia 100.
Nae Mkurugenzi mkuu wa tume ya Tehama Bw.Samson mwela amesema katika kongamano hilo wamezindua rasmi mfumo wa kusajili wataalamu wa tehama ambapo wametoa vyeti 100 kwa watalamu ili kuweza kusaidia taifa kujua idadi yao na kutambua uwezo wa ndani ya nchi katika maswala ya Tehama.
Na kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa kuendeleza sekta ya fedha Tanzania FSDT, Bw.Sostenes Kewe amesema lengo la kudhamini kongamano hilo ni pamoja na kutoa nafasi au fursa kwa wadau mbalimbali katika Tehama hapa nchini ili waweze kujadili, kutafakari na kubuni njia mbalimbali za kuhakikisha kwamba Tehama inaleta mageuzi ya kweli katika uchumi wa nchi hasa kumkomboa mwananchi mwenye maisha ya chini.