************************************
MGOMBEA ubunge Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James, amekutana na vijana wa Kata ya Kalebezo na kufanya mazungumzo nao juu ya kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu nchini.
Akiwa kwenye kikao hicho, Shigongo amewatia chachu na hasira vijana hao katika kuyasaka mafanikio kwa njia halali huku akiwaeleza kuwa vijana wana nguvu kubwa ya kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi wanaowaamini katika kuwaletea maendeleo.
Pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana wa Kata ya Kalebezo na Jimbo la Buchosa kwa jumla, Shigongo amesema lengo lake ni kuona vijana wanafanikiwa kiuchumi, hivyo akichaguliwa atazunguka jimbo nzima kufundisha vijana namna bora ya kutoka kiuchumi na amewaomba pindi semina hizo zikianza wajitokeze kupata mafunzo ya kujikwamua kutoka umasikini hadi kufikia utajiri.
Aidha, amewasihi kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo ili kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa taifa hili waliotangulia.
Akiwaomba kura, amesema siku zote amekuwa na nia ya dhati ya kuwatumikia vijana na wananchi wa Jimbo la Buchosa kila anapopata fursa hiyo hata kabla ya kugombea nafasi hiyo.
Kwa upande mwingine, amesema Rais John Magufuli anapaswa aongozewe miaka mingine mitano kutokana na utendaji wake usio na shaka ambapo amesaidia kuinua uchumi wa taifa letu kufikia uchumi wa kati kabla ya mwaka uliokuwa umepangwa wa 2025 huku akituongoza kumwomba Mungu na tukafanikiwa kulitokomeza janga la Corona liloyatesa mataifa makubwa duniani.