………………………………………………………………………..
Kiasi cha shilingi Bilioni 38 kitatumika kwaajili ya kukarabati upya miundombinu ya maji iliyoharibika na kuanzisha miundombinu mipya ili wananchi wa jimbo la Ilemela waweze kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.
Hayo yamebainishwa na mgombea ubunge wa jimbo la Ilemela kupitia CCM Dkt Angeline Mabula wakati akihutubia wananchi wa kata ya Nyasaka katika viwanja vya Senta Stendi ambapo amesema kuwa kero ya maji katika jimbo hilo inaenda kuwa historia hivyo kuwaomba kukiamini chama chake na kuchagua wagombea wa chama hicho kwa nafasi za Uraisi, Ubunge na Udiwani ili kero hiyo iweze kutatuliwa kwani Serikali ya Dkt John Magufuli imekwishatoa kiasi hicho cha fedha kwaajili ya kuimarisha miundombinu chakavu ya maji iliyokuwa ikichangia ukosefu wa maji ukilinganisha na idadi ya watu wanaohitaji huduma hiyo
‘.. Wana Nyasaka ni mashahidi Serikali imekwishatoa fedha kwaajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji iliyokuwa imeharibika na mnaona kazi inaendelea mkandarasi yupo kazini ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula akawaasa vijana kutumia fursa ya uwepo wa fedha za mikopo ya halmashauri kwa kujiunga katika vikundi na kukopa fedha hiyo kama mtaji wa kuanzisha shughuli za uzalishaji mali badala ya kukaa vijiweni na kulalamika bila kuchukua hatua yeyote.
Akimkaribisha mgombea huyo, Meneja kampeni wa jimbo la Ilemela Ndugu Kazungu Safari Idebe akawaomba wananchi wa kata ya Nyasaka kumchagua Rais Dkt John Magufuli na wasaidizi wake kutoka chama cha mapinduzi ili kazi ya kuleta maendeleo waliokwisha ianza iweze kukamilika kama ilivyokusudiwa badala ya kuchagua viongozi wasio na maono ya maendeleo kwa watu wanaotaka kuwaongoza.
Nae mbunge mteule wa umoja wa vijana UVCCM mkoa wa Mwanza Bi Ng’wasi Kamani mbali na kusisitiza amani na utulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa vijana na kuacha kutumika na baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema nchi akawaomba vijana kuhakikisha wanachagua wagombea wenye uwezo wa kuwaletea maendeleo ambao hawatoki chama kingine chochote isipokuwa CCM
Akihitimisha katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Isimbula akawahakikishia wananchi hao kuwa kama watachagua wagombea wa CCM utatuzi wa kero zao si jambo la kujadilika huku akiwaombea kura wagombea wa CCM kwa nafasi zote za uchaguzi.