Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na misako na doria katika maeneo mbalimbali na kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio ya uhalifu, ajali za barabarani na kukamata watuhumiwa wa matukio ya uhalifu. Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni:-
KUKAMATA SILAHA NA RISASI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kukamata silaha mbili zisizo kuwa na namba zilizotengenezwa kienyeji aina ya Short Gun na Pistol pamoja na risasi kumi [10].
Tukio hili limetokea mnamo tarehe 05.10.2020 majira ya saa 20:30 usiku huko katika barabara ya Mbeya – Tabora katika Kijij na Kata ya Mafyeko, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Polisi wakiwa doria waliwatilia mashaka watu wanne waliokuwa kwenye Pikipiki yenye namba za usajili MC 706 DCD Fekon ambao baada ya kuona gari ya Polisi walishuka na kutelekeza Pikipiki hiyo na begi dogo jeusi.
Aidha katika upekuzi uliofanyika katika begi hilo, kulikutwa bunduki mbili [02] zilizotengenezwa kienyeji aina ya short gun na pistol, panga mbili, shoka moja iliyo na mpini, tochi mbili. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako wa kuwatafuta watuhumiwa hao.
KUINGIZA BIDHAA NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia GETRUDA SHEKA [40] Mkazi wa Nzovwe akiwa ameingiza vitenge doti 21 bila kulipia ushuru.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 06.10.2020 majira ya saa 00:30 usiku huko Nzovwe, Kata ya Nzovwe, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Mtuhumiwa aliingiza bidhaa hizo kutoka nchi ya Malawi.
AJALI YA MOTO KUSABABISHA KIFO.
Mnamo tarehe 05.10.2020 majira ya saa 12:30 mchana huko Kitongoji cha Sholongo, Kijiji na Kata ya Swaya, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya. HILDA KILELA [66] Mkazi wa “Airport” ya zamani aliungua moto mwili mzima na kufariki dunia wakati akisafisha shamba lake. Chanzo ni moto kumzingira mhanga wakati akisafisha shamba. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu wa ajili ya mazishi.
AJALI YA MOTO KUUNGUZA GARI.
Mnamo tarehe 05.10.2020 majira ya saa 23:10 usiku huko maeneo ya Songwe “Airport”, Kata ya Nsalala, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Mbeya hadi Tunduma. Gari yenye namba ya usajili T.280 BYL aina ya Toyota Land Cruiser V8 mali ya Profesa. NORMAN SIGALA akitokea Sumbawanga kuja Mbeya Mjini ilishika moto kisha kuwaka na kuteketea lote.
Chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu katika mfumo wa umeme wa Gari hilo. Hakuna madhara kwa Dereva wala abiria waliokuwa kwenye gari hilo. Ufuatiliaji unaendelea.