Pia wamiliki wa shule hizo wameiomba serikali kusamehe kodi kwenye vifaa vya kubaini viashiria vya moto,kuzima na kudhibiti majanga ya moto yanapotokea kwenye shule zao ili waviagize kutoka nje ya nchi.
Uamuzi huo ulifikiwa jana baada ya kupokea taarifa ya uongozi wa BAKWATA ya ukaguzi wa miundombinu ya shule zinazomilikiwa na taasisi za kiislamu ili kubaini kasoro ama mapungufu kwenye shule hizo kutokana na kukumbwa na matukio ya majanga ya moto.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA, Shaaban Moshi alisema shule walizotembelea nyingi hazina vifaa vya kubaini viashiria vya moto na vya kuzima moto na zenye vifaa havikidhi,hakuna vituo vya kujiokolea,milango ya kuingia na kutoka mabwenini na miundombinu ya umeme si rafiki inapotokea ajali ya moto ama dharura.
Kwa muktadha huo wamiliki na waendeshaji wa shule hizo wametakiwa kuboresha miundombinu hiyo lakini pia kupata mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto yanapotokea.
Naye Mkurugenzi wa Islamic Development Founadation (IDF) Juma Chia alisema silaha pekee ya kukabiliana na majanga ya moto shuleni, wamiliki na BAKWATA wakutane ili kuweka mikakati thabiti ya kumaliza tatizo hilo na liundwe jukwaa la wamiliki wa shule za Kiislamu na wadau wa elimu ambalo litasaidia kukabiliana na majanga hayo na changamoto za elimu.
“Zipo ajali za moto za hujuma na zingine za uzembe wa kibinadamu,kama shule yaliyo ndani ya wajibu wetu tuyafanye kwa kuweka vifaa vya kubaini na kuzima moto, pia ushirikiano wa wataalamu wa Jeshi la Zimamoto na Tanesco, watoe elimu kwa walinzi, wanafunzi,walimu na walezi ili wapate maarifa ya kutambua viashiria vya moto shuleni,”alisema Nchia.
Pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA), Mkuu wa mkoa mstaafu Amina Masenza,alishauri ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa majanga ya moto ufanyike ukaguzi wa mifumo ya nyaya za umeme kuona kama imeathiriwa ,kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi wasishiriki hujuma za moto.
Mjumbe wa Bodi ya Shule ya Thaqaafa,Idrisa Haeshi,yeye alishauri kila shule ianishiwe mapungufu yaliyopo kwenye miundombinu ya majengo,mifumo ya nishati ya umeme,vifaa na kupewa muda wa kuboresha ili kuepuka athari za majanga ya moto.
Aidha Makamu Mwenyekiti wa wa Bodi ya Shule ya Muntazir, Yahya Lushaka,sababu za kubuka kwa majanga ya moto hazijapatikana kwa usahihi ingawa ajali zingine ni hujuma hivyo zifanyike jitihada za kudhibiti hali hiyo huku taasisi husika zikijenga uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto shuleni.
Akizungumza baada ya taarifa na kupokea mapendekezo ya wadau hao, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Alhaji Sheikh Hasani Kabeke alisema,licha ya mapungufu wamebaini watumishi wa mamlaka za elimu wanatumia lugha isiyofaa na kuchelewa kutoa vibali vya uanzishaji wa mabweni na bodi za shule.
Alisema jambo hilo linahusu mstakabali wa maisha ya Waislamu na watoto wao hivyo ni muhimu kujenga mshikamano kwa shule za Kiislamu kuondoa mambo yaisyofaa na wakishikamana watapiga hatua kwa kasi kubwa.
“Tunafurahi baada ya ukaguzi uliofanywa na BAKWATA baadhi ya shule zimeboresha miundombinu yenye kasoro, hivyo tuendelee kuwa na subira na watulivu wakati na baada ya majanga ya moto ili kutoa fursa kwa serikali na vyombo vyake kuchunguza ili mwishowe tupate taarifa sahihi ya vyanzo vya kadhia hiyo,”alisema Sheikh Kabeke.
Alisistiza wamiliki kuhakikisha kasoro zilizobainika wazifanyie kazi harak ili kunusuru maisha ya watoto na majanga ya moto ambapo BAKWATA itakuwa ikifanya ukaguzi mara mbili kwa mwaka kwenye taasisi hizo za elimu zinazomilikiwa na Waislamu.