Na Mwandishi Wetu DAR ES SALAAM
TIMU ya Azam FC imefanikiwa kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 4-2 dhidi ya Kagera Sugar usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa mara nyingine tena, mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Mpumelelo Dube ameibuka shujaa wa Azam FC leo baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi huo dakika ya sita na 88.
Mabao mengine ya Azam FC inayofundishwa na kocha Mromania, Aristica Cioaba yamefungwa na washambuliaji wengine wa kigeni, Mzambia Obrey Chirwa dakika ya 48 na Muivory Coast dakika ya 51.
Kwa ushindi huo, Azam FC inaendeleza rekodi yake ya asilimia 100 na kufikisha pointi 15 baada ya kucheza mechi tano, ikiwazidi pointi mbili vigogo, Simba na Yanga wanaofuatia.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, mabingwa watetezi, Simba SC wameshinda 4-0 dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, mabao ya Meddie Kagere mawili, Chriss Mugalu na Luis Miquissone moja kila mmoja.
Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza bao pekee la Kelvin Friday dakika ya tisa limewapa ushindi wa 1-0 wenyeji, Biashara United dhidi ya Mtibwa Sugar.
Na Raundi ya tano itahitimishwa leo kwa mchezo mmoja, kati ya KMC na Polisi Tanzania Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.