Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) Mhandisi Gibon Nzowa (kulia) akisikiliza swali kutoka kwa mtaalam wa mazingira wa Wizara ya Maji Mhandisi Peter Kishiwa, kuhusu ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji katika mradi wa maji wa Muze, uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Mfumo wa kuchuja maji katika mradi wa maji wa Muze, uliopo Halmashauri ya Sumbawanga. Mradi huo utahudumia jumla ya vijiji 10 na katika mwambao wa Ziwa Rukwa na tayari baadhi vimeanza kunufaika na mradi, wakati kazi ikiendelea kufikisha mtandao wa maji kwa wananchi wengine.
Mkurugenzi Msaidizi, Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maji Bw. Alex Tarimo (katikati) akimtua mama ndoo Kichwani , Bi. Lucia George mkazi wa Kijiji cha Kalumbaleza. Kijiji hicho ni moja ya maeneo ambayo tayari yanafaidika na mradi wa maji wa Muze ambao unatekelezwa kwa kutumia wataalam wa Wizara ya Maji kwa utaratibu wa force account.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) Mhandisi Gibon Nzowa akiangalia moja ya kituo cha kuchota maji kilichofanyiwa uharibifu katika shule ya msingi Kalumbaleza. Pamoja na kuhudumia wananchi, kituo hicho kinatoa huduma ya majisafi na salama kwa jumuiya ya shule hiyo na wanafunzi zaidi ya 500.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kalumbaleza, Halmashauri ya Sumbawanga wakiwa na furaha baada ya kupewa ahadi na Mkurugenzi Mtendaji wa SUWASA Mhandisi Gibon Nzowa kuwa huduma ya maji itarejeshwa shuleni hapo ndani ya saa sita, baada ya waharibifu kubomoa mfumo wa majisafi katika kituo cha kuchota maji katika shule yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) Mhandisi Gibon Nzowa akiwa katika kikao cha dharura na wanafunzi pamoja na jumuiya ya shule ya Msingi ya Kalumbaleza, Halmashauri ya Sumbawanga, kujadili utunzaji wa miundombinu ya maji na matumizi sahihi ya vituo vya kuchota maji. Kikao hicho kimefanyika baada ya uharibifu kufanyika katika kituo cha kuchota maji na kusababisha adha kwa wanafunzi wa shule hiyo.
…………………………………………………………………………
Mkoa wa Rukwa umeongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi kutoka asilimia 40.1 iliyokuwepo mwaka 2016 hadi kufika asilimia 71. Ongezeko hilo limechangiwa na miradi ya maji iliyotekelezwa na wataalam wa Wizara ya Maji kwa kutumia utaratibu wa force account.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Rukwa Mhandisi Boaz Matundali amesema jumla ya miradi ya maji 30 imekamilishwa maeneo ya vijijini na wananchi wanapata huduma.
“Miradi mingine 39 inaendelea na ipo katika hatua mbalimbali katika wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi” Mhandisi Matundali ameainisha na kuongeza kuwa miradi hiyo inatekelezwa kupitia mpango wa Lipa kwa Matokeo (PforR), Lipa kwa Matokeo (PbR) na uwezeshaji wa Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF).
Ameongeza kuwa mkakati uliopo hivi sasa ni kuhakikisha wananchi katika idadi ya vijiji 124 wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza kwa shughuli mbalimbali za kila siku.
Mhandisi Matundali amesema kwa upande wa mjini Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA) inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji katika mji mdogo wa Laela, Nyamanyele, Muze na Kirando, ambapo wananchi wameshaanza kupata huduma kwa baadhi ya maeneo, wakati kazi ikiendelea ya kuweka mtandao kuwafikia wengine.
Mkoa wa Rukwa upo chini ya Bonde la Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika na unayo maabara ya maji kwa ajili ya kusimamia ubora wa maji na kutoa taarifa za hali ya ubora wa maji.