Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, akizungumza na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara husika (kulia) pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (kushoto), wakati Ujumbe huo ulipozuru Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani ili kujionea maendeleo yake
Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), wakikagua miundombinu mbalimbali inayoendelea kujengwa katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani. Ujumbe huo ulitembelea Mradi husika, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (katikati), akiwa na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), wakati Ujumbe huo ulipotembelea Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani, Oktoba 03, 2020ili kujionea maendeleo yake.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB) baada ya Ujumbe huo kuhitimisha ziara yake katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani, Oktoba 03, 2020, iliyolenga kujionea maendeleo yake.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Board – REB), Wakili Julius Kalolo, akizungumza neno, wakati Bodi hiyo (kushoto) na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati (kulia), walipotembelea Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji, mkoani Pwani, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake. Wa kwanza kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja.
Mhandisi Mkazi wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Mushubila Kamuhabwa, akitoa wasilisho la Mradi huo kwa Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati (kulia) pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (kushoto), walipozuru Mradi huo, Rufiji mkoani Pwani, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.
Ujenzi wa miundombinu mbalimbali ukiendelea katika Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji, mkoani Pwani. Taswira hii ilichukuliwa Oktoba 03, 2020 wakati Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (hawapo pichani), walipozuru Mradi huo ili kujionea maendeleo yake.
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutembelea Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji mkoani Pwani, Oktoba 03, 2020 ili kujionea maendeleo yake.
………………………………………………………………
Veronica Simba – Rufiji
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja, amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kuwaamini wazalendo katika kusimamia utekelezwaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).
Alitoa pongezi hizo Oktoba 3, 2020 wakati akizungumza na Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara ya Nishati pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REB), waliotembelea Mradi huo unaotekelezwa wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, ili kujionea maendeleo yake.
Mhandisi Masanja alisema kuwa hatua ya Mheshimiwa Rais kuwaamini wataalamu wazalendo kusimamia usanifu wa awali, hatua za manunuzi na hata usimamizi wa utekelezaji wa mradi wenyewe, pasipo kushirikisha wataalamu wa kigeni ni ushahidi kuwa Tanzania ina hazina ya wataalamu mahiri.
“Kupitia Mradi huu, tumeudhihirishia ulimwengu kuwa Tanzania ina wataalamu mahiri na kwamba sisi wenyewe tunaweza kusimamia miradi yetu.”
Akifafanua, alieleza kuwa Serikali iliamua kuwatumia wataalamu kutoka TANROADS (TANROADS Engineering Consulting Unit – TECU) kama Mshauri Mwelekezi wa Mradi na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kama wawakilishi wa Serikali katika kusimamia Mradi husika ili kuhakikisha Mkandarasi anatekeleza kazi zote kwa mujibu wa Mkataba.
Aidha, aliongeza kuwa, jambo la kujivunia zaidi ni kuwa Mradi huo unatekelezwa na fedha za Serikali kwa asilimia 100, hivyo akawataka Watanzania kujivunia Mradi huo kwani nchi inaumiliki kikamilifu.
Awali, akitoa wasilisho la Mradi kwa Ujumbe husika, Mhandisi Mkazi wa Mradi huo, Mushubila Kamuhabwa, alisema kuwa katika hatua ya ujenzi inayoendelea sasa, Mradi umewezesha uzalendo na mshikamano wa hali ya juu kwa vijana wa kitanzania wanaofanya kazi za ujenzi.
“Ni kama wakati ule vijana walipokuwa wakishiriki mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa. Utawakuta vijana hawa wakiimba nyimbo za kizalendo wakati wanafanya kazi na pia wakishirikiana kwa kila jambo, hali inayoonesha wazi wanajisikia fahari kuwa sehemu ya utekelezaji wa Mradi huu.”
Vilevile, Mhandisi Kamuhabwa alibainisha kuwa miongoni mwa waajiriwa 5,500 wa Mradi waliopo sasa, Watanzania ni 4,900 ambao ni takribani asilimia 90 ya waajiriwa wote, jambo ambalo linadhihirisha dhamira ya Serikali kuhakikisha Watanzania wanapewa kipaumbele katika kila sekta ya Mradi huo.
Aidha, alibainisha faida nyingine ambazo zimekwishaanza kupatikana katika hatua hii ya awali ya utekelezaji wa Mradi kuwa ni pamoja na matumizi ya rasilimali za ndani ya nchi kama vile nondo, saruji, vyakula, ulinzi na nyinginezo.
Kuhusu faida zitakazopatikana baada ya kukamilika kwa Mradi, alisema pamoja na kuzalisha umeme mwingi utakaokuwa na bei nafuu, Mradi huo pia utakuza sekta za utalii, kilimo, uvuvi wa samaki pamoja na kuboresha mazingira kutokana na kupungua kwa ukataji miti kwa matumizi ya mkaa na kuni.
Alitaja faida nyingine kuwa ni kudhibiti mafuriko kwa kudhibiti maji ya Mto Rufiji ambayo awali yalikuwa yakileta majanga ya kuua watu na kuharibu mali zao.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, Mwenyekiti wake, Wakili Julius Kalolo alipongeza kazi inayofanyika ambapo alisema yeyé na wenzake wameridhishwa na kasi pamoja na viwango katika utekelezaji huo wa Mradi.
Aliongeza kuwa pindi Mradi huo utakapokamilika utaongeza nguvu zaidi kwa Wakala huo kufikisha umeme kwa kila kaya, ikizingatiwa kuwa tayari taasisi hiyo imeanza utekelezaji wa kupeleka umeme katika kila kitongoji nchini.
Naye Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Edward Ishengoma alisema kuwa Wizara iliona umuhimu wa kuandaa ziara hiyo kwa ajili ya Wajumbe wa Menejimenti yake, ili kuwawezesha kujionea kwa macho kinachofanyika ikizingatiwa kuwa ndiyo Wizara Mama inayohusika na Mradi huo.