…………………………………………………………………………..
Mbaraka Kambona, Tanga
Mapato ya Halmashauri ya Mkinga, Mkoani Tanga kupitia Sekta ya Uvuvi yamepanda kufikia shilingi Milioni 96.6 mwaka 2019/ 2020 kufuatia mikakati waliyoiweka dhidi ya Uvuvi haramu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga, Rashid Gembe wakati akiongea na timu ya Wataalamu kutoka Mradi wa Ulinzi Shirikishi wa rasilimali za bahari kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (SWIOfish) ofisini kwake mwishoni mwa wiki alisema kuwa kabla ya mradi huo kuanza kuhamasisha uvuvi endelevu na wenye tija, mwaka 2015/ 2016 Halmashauri ya Mkinga ilikusanya kiasi cha shilingi Milioni 45.3 kutoka katika sekta ya Uvuvi.
Gembe aliwaeleza wataalamu hao waliokwenda kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo Wilayani humo kuwa mradi umechangia kwa kiasi kikubwa kukomeshwa kwa uvuvi haramu hususani uvuvi wa kutumia mabomu na makokoro.
“Mradi wa SWIOfish ulipoanza kufanya kazi hapa Wilayani kwetu mwaka 2016 ulianzisha Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Bahari (BMU) zipatazo 14 ambazo zimesaidia kutoa elimu ya ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwa wananchi ikiwemo kutunza mazingira ya fukwe za bahari”,alisema Gembe
“Pamoja na kuimarisha BMU hizo, pia iliimarisha Doria za Baharini na nchi kavu kwa lengo la kulinda rasilimali za uvuvi, na nikiri kuwa Doria hizo zimesaidia kupungua kwa uvuvi haramu na sasa mapato ya Halmashauri yameanza kupanda kwa sababu wavuvi sasa wanafanya uvunaji endelevu wa rasilimali za uvuvi”,aliongeza Gembe
Kufuatia mafanikio hayo, Gembe aliuomba mradi wa SWIOfish kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi katika mwambao wa bahari wilayani humo ili rasilimali za uvuvi zilizopo ziendelee kuwanufaisha waliopo na vizazi vijavyo.
Aidha, aliwasihi wananchi wanaoishi katika mwambao wa bahari waliopata elimu hiyo ya utunzaji wa rasilimali za bahari na uoto wake waendelee kuienzi elimu hiyo kwa kuisambaza kwa wengine ili rasilimali hizo ziendelee kunufaisha jamii hizo na Taifa kwa ujumla.
“Niwatake wananchi kuacha kukata mikoko na waendelee kuwa sehemu ya ulinzi wa rasilimali za uvuvi ili ziendelee kuwa na tija kwa jamii”,alisisitiza
Aliwakumbusha wananchi wa Wilaya hiyo kuwa mapambano dhidi ya uvuvi haramu sio nguvu ya soda ni mapambano endelevu na hawatakuwa na huruma na yeyote atakaye kwenda kinyume.
“Wananchi watambue kuwa tunafanya haya kwa nia njema, sisi tutaondoka lakini hii nchi itaendelea kuwepo, tufikirie Tanzania ya miaka 50 ijayo, tusiwe na mawazo ya kupata sasa tu, huo utakuwa ubinafsi”,alifafanua Gembe
Mkurugenzi huyo aliushukuru mradi wa SWIOfish kwa kuwapatia vifaa mbalimbali ambavyo vimeweza kuisaidia halmashauri hiyo kuvitumia katika kulinda rasilimali za bahari.
Mwisho.
Maelezo ya Picha.
Wataalamu kutoka Mradi wa Ulinzi Shirikishi wa rasilimali za bahari kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (SWIOfish) wakiwa katika picha ya pamoja na Wanachama wa Kikundi cha Hiari ya Moyo kilichopo katika Kijiji cha Msaraza, Wilayani Pangani Mkoani Tanga walipokitembelea kufuatilia maendeleo yake mwishoni mwa wiki. Wa kwanza kulia ni Afisa Mawasiliano wa mradi, Amina Kiaratu na wa Kwanza kushoto ni Afisa Ufuatiliaji na Utathimini wa Mradi, Furaha Kabuje.