………………………………………………………………..
Kiasi cha shilingi bilioni 28 kitatumika kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi na malori inayojengwa katika kata ya Nyamhongolo wilaya ya Ilemela ili kukuza uchumi na kupunguza changamoto ya ajira.
Hayo yamebainishwa na Naibu waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi ambae pia ni mgombea ubunge wa jimbo la Ilemela kupitia chama cha mapinduzi Dkt Angeline Mabula wakati alipotembelea stendi hiyo kufuatilia utekelezaji wa mradi huo kabla ya kuzungumza na wananchi wa kata ya Nyamhongolo katika muendelezo wa mikutano yake ya kampeni kueleza juu ya miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano ambapo amesema kuwa mradi huo wa stendi ya kisasa umeweza kuajiri zaidi ya watu 206 wenye utaalamu na wasio na ujuzi rasmi huku akiwaomba wananchi wa kata hiyo kutumia fursa ya uwepo wa mradi huo kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara na kuanzisha miradi mingine ndani na jirani ya stendi hiyo
‘ Tujiandae tukawekeze pale kwenye mradi ule wa stendi utakapokamilika, tusiogope tuombe vyumba vya biashara ‘ Alisema
Aidha Dkt Mabula akaongeza kuwa amefurahishwa na uwepo wa mkakati wa ujenzi wa eneo la kufanyia biashara wajasiriamali wadogo wadogo maarufu kama machinga jirani na stendi hiyo jambo litakalosaidia kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima kama inayojitokeza maeneo mengi ya mijini kutokana na kukosekana kwa maeneo rasmi ya wafanya biashara hao.
Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo Mhandisi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Juma King’ora akafafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Mei na mpaka sasa umeshafikia asilimia 52 ya utekelezaji wake.
Huku msanifu majengo ambae pia ni msimamizi msaidizi wa mradi huo Ndugu Hellen Mgalula akisema kuwa mradi huo ulitarajiwa kukamilika mapema zaidi kabla ya muda uliopangwa sasa lakini changamoto za kuzuka kwa ugonjwa wa homa ya mafua makali inayojulikana kama Covid-19 na uwepo wa maji mengi eneo la mradi umechangia kuongeza siku za kukamilika kwake.