Mkazi wa Bomani Mkoani Manyara,Moita Tepeno akiwa ofisi za TAKUKURU baada ya kuomba rushwa kwa raia mwemaakidai anapeleka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto ili asichukuliwe hatua kutokana na mtoto wake kupata ujauzito.
***************************************
Na Mwandishi wetu, Kiteto
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU inamshikilia mkazi wa mtaa wa Bomani Mkoani Manyara, Moita Tepeno kwa kujipatia fedha kwa kutumia jina la Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Kanali Patrick Nobert Songea.
Tepeno anashikiliwa na TAKUKURU kwa kujipatia shilingi 500,000 kwa njia ya udanganyifu kinyume na kifungu Cha 302 kikisomwa pamoja na kifungu cha 301 vyote vya sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Joseph Holle Makungu amesema Tepeno alikamatwa Octoba 2 mwaka huu kwenye eneo la Bomani baada ya kunaswa katika mtego wa rushwa kwa kupokea shilingi 500,000.
Makungu amesema awali TAKUKURU walipata taarifa kutoka kwa raia mwema jina linahifadhiwa kuwa Tepeno anatumia vibaya jina la mkuu wa Wilaya ya Kiteto kanali Songea.
Amesema Tepeno alimueleza raia mwema huyo kuwa alitakiwa kupeleka kwa Mkuu huyo wa wilaya shilingi 500,000 ili asichukuliwe hatua baada ya binti yake kupata ujauzito na kushindwa kwenda shule.
“Raia huyo mwema ni kweli alikiri mtoto wake wa kike ni mjamzito alikuwa anasoma Mkoani Arusha ila akapata tatizo hilo akiwa Kiteto kwenye likizo ndefu ya homa ya Corona,” amesema Makungu.
Amesema mzazi huyo baada ya kutakiwa kutoa kiasi hicho cha fedha alitoa taarifa TAKUKURU na kukamatwa na atafikishwa mahakamani pindi taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Amesema TAKUKURU inawasihi watumishi wote na wananchi kwa ujumla kuacha tabia ya kutumia majina ya viongozi katika ngazi yoyote kwa lengo la kujipatia manufaa yoyote kwani kitendo hicho licha ya kuwachafua viongozi kinawachonganisha wananchi na viongozi wao.