Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Suleiman Mzee akieleza jambo wakati Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde (hayupo pichani) alipofika Ofisini kwake katika ziara ya kikazi yenye malengo ya ufuatiliaji wa maandalizi ya Mfumo wa Ushirika katika msimu mpya wa Korosho 2020/21, hivi karibuni Mkoani Mtwara.
Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw. Charles Malunde akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Newala wakati wa Ziara ya kikazi yenye malengo ya ufuatiliaji wa maandalizi ya Mfumo wa Ushirika katika msimu mpya wa Korosho 2020/21
Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Joseph Mmole akisoma taarifa za Chama hicho wakati wa kikao cha tathmini na maandalizi ya msimu mpya wa Korosho katika masuala ya Ushirika, Kikao kilichuhudhuriwa na Naibu Mrajis Charles Malunde, Maafisa Ushirika na Wajumbe wa Bodi MAMCU Wilayani Masasi Mkoani Mtwara
Washiriki wa kikao cha tathmini na maandalizi ya msimu mpya wa Korosho wakiwemo Maafisa Ushirika, Wajumbe wa Bodi na Menejimenti ya MAMCU Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara
………………………………………………………………..
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Suleiman Mzee ametoa wito kwa Viongozi, Watendaji na Wasimamizi wa Sekta ya Ushirika kuhakikisha Wakulima wanapata fursa ya kuhakiki Akaunti zao za Benki kama maandalizi muhimu ya msimu mpya wa Korosho 2020/21 ili kuondokana na changamoto za uchelewaji wa malipo ya Wakulima.
DC ametoa wito huo wakati Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Bw.Charles Malunde alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Wilaya Masasi Mkoani Mtwara katika ziara ya kikazi hivi karibuni katika maandalizi ya Msimu mpya wa Korosho kwa upande wa masuala ya Ushirika. Hivyo, kutathmni msimu uliopita ili kuangalia namna bora ya kuondokana na changamoto zilizojitokeza kwenye Vyama vya Ushirika kwa maboresho zaidi ya msimu mpya.
`Mkuu huyo amesema baadhi ya Changamoto ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara ni pamoja na uchelewaji wa malipo ya wakulima. Hivyo, amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na Mabenki kuratibu zoezi la wakulima kuhakiki taarifa zao muhimu kama vile majina sahihi, namba za Akaunti na taarifa nyinginezo mwanzo wa msimu ili kuondosha uwezekano wa Wakulima kuchelewa kupata malipo yao baada ya mauzo.
“Mkulima apate taarifa kwenda kuhakiki taarifa zake za Benki ili kama kuna dosari yoyote ipate ufumbuzi mapema kabla ya minada ya mauzo kuanza ili hatimaye apate malipo yake kwa wakati,” alisema DC
Aidha, Mhe. Suleiman Mzee amewataka Viongozi wa Ushirika kuendelea kuusimamia na ubora wa Korosho zinazokusanywa na Wakulima katika Vyama vyao. Aliongeza kuwa ubora huo huanzia hatua za awali kuanzia shambani hadi kufikia Ghalani kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na zinazotolewa na Maafisa Ugani pamoja na Viongozi wa Ushirika.
Katika hatua nyingine, Naibu Mrajis Malunde katika kikao na Maafisa Ushirika, Viongozi na Wajumbe wa Bodi wa Chama Kikuu ca Ushirika Masasi Mtwara (MAMCU) Wilayani Masasi ameshauri kuangalia uwezekano wa kusimamia Amcos kujishughulisha na mazao mengi zaidi kwa kadri ya rutuba na hali ya hewa inavyoruhusu.
Alieleza kwa kufanya hivyo kutapanua wigo wa biashara kwa vyama vya msingi kutokana na uzalishaji wa mazao mbalimbali yatakayokuwa yakitoka kwa wakulima. Alifafanua zaidi kuwa mbali ya zao la Korosho vilevile Wakulima wahamasishwe katika kilimo cha mazao kama vile Ufuta, mbaazi na Choroko. Hivyo, kuongeza mapato na ufanisi wa Vyama vya Ushirika.
Naibu Mrajis amewataka Maafisa Ushirika, Menejimenti na Wajumbe wa Bodi kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na misingi ya Ushirika. Akisisitiza utendaji wenye kuzingatia maadili na uadilifu hasa tunapoelekea kwenye kipindi cha msimu mpya wa Korosho.
Mwisho