Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Jairy Khanga kushoto akiwasikiliza jana wajumbe wa kamati ya ujenzi wa kituo cha Afya Magagura katika halmashauri ya wilaya Songea inayojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 400 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 90.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Jairy Khanga wa mbele kushoto akikagua miundombinu ya ujenzi wa kituo cha Afya Magagura halmashauri ya wilaya Songea ambayo itakapokamilika itasaidia kusogeza huduma za matibabu kwa wananchi na kuboresha afya za wakazi wa kata ya Magagura na maeneo ya jirani,wengine ni wajumbe wa kamati ya ujenzi.
Picha na Muhidin Amri
***********************************
Na Muhidin Amri,
Songea
SERIKALI imeupatia mkoa wa Ruvuma shilingi bilioni 12.3 kwa ajili ya kuboresha huduma na kuimarisha miundombinu ya Afya katika mkoa huo katika kipindi cha miaka minne kutoka 2017 hadi 2020.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dkt Jairy Khanga, amesema hayo jana mara baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya Magagura katika halmashauri ya wilaya ya Songea ambacho hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 90.
Dkt Khanga alisema,kupitia fedha hizo mkoa wa Ruvuma umeweza kujenga vituo 25 vya kutolea huduma ya afya ikiwemo Hospitali 4 katika wilaya ya Nyasa,Namtumbo,Tunduru na Songea,vituo vya afya 16 na zahanati 5 ambazo zimesaidia sana kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.
Alisema, kati ya fedha hizo halmashauri ya wilaya ya Songea imepata shilingi bilioni 3.5 ambazo zimewezesha kujenga vituo vya Afya 3 vya Muhukuru,Magagura na Matimila kwa gharama ya shilingi bilioni 1.3,zahanati 4 kwa shilingi milioni 400 na Hospitali ya wilaya1inayojengwa katika kijiji cha Mpitimbi ambayo ujenzi wake umetengewa shilingi bilioni 1.8.
Alisema, gharama ya ujenzi wa kituo cha Magagura ni shilingi milioni 400 ambazo zinahusisha majengo 4, ambayo ni maabara,jengo la mama na mtoto,jengo la wagonjwa wa nje(OPD) na upasuaji, lakini kutokana na ushiriki mkubwa wa wananchi fedha hizo zimewezesha kuongeza kujenga choo cha wagonjwa wa nje,kichomea taka na shimo la choo.
Alisema, kujengwa kwa kituo cha Afya Magagura kimsingi itasaidia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi hasa ikizingatia kuwa wakazi wa kijiji hicho kwa muda mrefu walilazimika kwenda hadi zahanati ya misheni Chipole kufuata matibabu.
Dkt Khanga, amewapongeza sana wananchi wa kata ya Magagura kwa ushirikiano waliotoa wakati wote wa ujenzi wa kituo hicho na kuwataka kuendelea kushirikiana na serikali yao katika ujenzi wa miradi mingine inayolenga kuchochea maendeleo.
Amewataka watumishi watako pangiwa kwenda kufanya kazi katika zahanati na vituo vinavyojengwa kuhakikisha wanawahudumia wananchi na kwenda kutoa huduma bora na ameonya kujiepusha kutoa lugha mbaya kwa wananchi watakaofika kupata huduma za matibabu.
Aidha, ametoa wito wananchi wa kata ya Magagura na mkoa wote wa Ruvuma kwenda kupata huduma za matibabu katika zahanati na vituo vya afya vinavyoendelea kujengwa kwa kuwa serikali imeleta wataalam na dawa za kutosha kwa ajili yao.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliokutwa wakishiriki ujenzi wa kituo hicho wameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa juhudi kubwa inayofanya katika kuboresha na huduma za afya hapa nchini.
Eliud Mtewele amesema, kujengwa kwa kituo cha afya Magagura kutachochea mambo mengi ya maendeleo ambayo hapo awali hayakuwepo kwa kuwa wakati mwingine wananchi walilazimika kwenda hospitali ya rufaa songea mjini na hospitali ya St Joseph Peramiho kufuata huduma za afya.
Jenista Komba mbali na kuishukuru serikali kwa kujenga kituo cha afya Magagura amesema, kituo hicho kitasaidia kuokoa maisha ya wanawake wengi wajawazito ambao wanapohitaji kujifungua walilazimika kutumia usafiri wa pikipiki na baiskeli kwenda hospitali ya mkoa hivyo baadhi yao kupoteza maisha wakiwa barabarani kabla ya kufika katika vituo vya kutolea huduma.